IMANI potofu zinadaiwa kutumiwa na watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji ili wapewe kinga wasikamatwe.
Diwani wa kata ya Manchali, Mary Mazengo alisema hayo juzi wakati wa mkutano uliowahusisha viongozi wa wilaya, madiwani, watendaji wa vijiji na kata ulioandaliwa na Shirika lisilokuwa na Kiserikali linalojihusisha na utetezi wa wanawake na watoto la Woman Wake Up (Wowap).
Alisema baadhi ya watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi wamekuwa wakikimbilia kwa waganga wa kienyeji ili wapate kinga wasikamatwe ambapo huko hutaja majina ya watu waliokuwa wakiwafuatilia.
“Imani potofu imekuwa ikiingia katika ufuatiliaji wa watia mimba kwa wanafunzi kwa baadhi ya maeneo watu wanakwenda kwa waganga wa kienyeji na kuwataja wanaowafuatilia,” alisema. Alisema hilo ni tatizo kubwa katika maeneo ya vijijini na elimu zaidi inahitajika ili imani hiyo isitumike katika kuharibu maisha ya wasichana wadogo ambao wana ndoto za kujiendeleza kielimu.
Alisema viongozi wana wajibu wa kuhakikisha wanawafuatilia watuhumiwa ili wafikishwe kwenye mikono ya sheria na si kutishika na wanaotumia imani hizo kuwa kama kinga kwao ili wasikamatwe. Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai alisema elimu imekuwa ikitolewa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye majukwaa kama vile mikutano ya vijiji, magulio, sherehe za kimila, mikutano ya vijana, matukio ya michezo na kutoa elimu ya haki za binadamu, jinsia na ukatili wa kijinsia.IMEANDIKWA NA SIFA LUBASI-HABARILEO CHAMWINO
Social Plugin