Tanzania na Misri zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika maeneo makuu 10, ikiwemo kuimarisha uhusiano, ulinzi na kujenga kiwanda kikubwa cha nyama pamoja na kiwanda cha dawa nchini.
Pamoja na makubaliano hayo ya kiuchumi na kijamii, suala la matumizi ya maji ya Mto Nile halijapatiwa muafaka na mazungumzo yanaendelea kuwezesha kukamilisha matumizi yenye faida ya mto huo kwa nchi zote zinazohusika.
Aidha, Misri imempongeza Rais John Magufuli kwa utawala mzuri kwa namna anavyopambana na rushwa na ufisadi na kufafanua kuwa nchi hiyo (Misri) inaendelea kushirikiana na Tanzania katika mapambano hayo.
Makubaliano hayo takriban 10 yalielezwa jana Ikulu, Dar es Salaam na marais hao wawili wa Tanzania, Dk Magufuli na wa Misri, Abdel Fattah Al Sisi wakati wakizungumza na waandishi wa habari.
Rais Magufuli alisema wamekuwa na mazungumzo marefu mara baada ya Rais Al Sisi kuwasili jana mchana na ziara hiyo ikifanyiwa kazi kwa yale waliokubaliana, italeta manufaa makubwa kwa nchi hizo mbili.
“Tumezungumza mengi leo, nchi ya Misri ina historia kubwa katika dunia ya sasa, ustaarabu wa maisha ya binadamu ukiachia mbali binadamu wa kwanza inaelezwa aliishi Tanzania (Olduvai Gorge), wasanifu majengo wa kwanza waliishi Misri, ushahidi upo hata leo pyramids leo bado hakuna anayeweza kuzijenga.
“Vitabu vitakatifu vinaandika kuhusu Misri, Mtume Yesu alikimbilia Misri alipotaka kuuawa, ni eneo la kukimbilia wenye shida na sisi tutakimbiza shida zetu kwao ili atusaidie kuzitatua,” alisema Dk Magufuli.
Alisema pamoja na kwamba hatujapakana kimipaka na Misri, lakini maji ya Mto Nile yameziunganisha nchi hizo mbili kwani chanzo cha maji kwenda Mto Nile ni pamoja na Mto Kagera na maji ya Ziwa Victoria ambalo asilimia 51 lipo Tanzania, 44 Uganda na tano Kenya.
Makubaliano
Akielezea kuhusu maeneo ya makubaliano, Rais Magufuli alisema kwanza kutokana na historia ya mahusiano mema na ya muda mrefu baina ya Baba wa Taifa wa nchi hizo mbili; Mwalimu Julius Nyerere na Gamal Abdel Nasser, wamekubaliana kuimarisha mahusiano hayo kwa mustakabali wa nchi hizo mbili.
Dk Magufuli alisema wamekubaliana kuunda upya Kamisheni za Kudumu za Kiuchumi za Pamoja baina ya Tanzania na Misri ,ambazo ziliundwa awali na waasisi hao (Nyerere na Abdel Nasser) wa nchi hizo mbili. “Tumekubaliana hizi kamati (kamisheni) za kudumu ziundwe upya, wakutane mawaziri wan chi hizi mapema,” alisema Magufuli.
Eneo jingine ni kukuza biashara kati ya nchi hizo ambapo alisema kwa kuwa Misri inahitaji nyama na Tanzania ni nchi ya pili kwa mifugo mingi, nchi hiyo (Misri) itajenga kiwanda kikubwa cha nyama nchini ili wasafirishe nyama yenye viwango bora kwenda Misri.
Kiwanda hicho kikikujengwa, ajira kwa Watanzania zitapatikana, mapato na wafugaji watapata kipato zaidi kwa kuuza nyama moja kwa moja katika kiwanda hicho. Katika eneo la biashara, kwa sasa kiwango cha biashara baina ya Misri na Tanzania ni Dola za Marekani milioni 78.02.
Kiwango ambacho jana Rais Magufuli alisema ni kidogo na kinahitajika kuongezeka. Rais pia alieleza kuwa, Misri imekubali kuleta nchini teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji nchini ili kukuza sekta ya kilimo.
Asilimia 95 ya nchi ya Misri ni jangwa na asilimia tano pekee huitumia kwa kilimo hasa cha umwagiliaji.
Alielezea eneo jingine kuwa ni sekta ya afya, ambapo amesema wamekubaliana na Rais Al Sisi kuendelea kuleta wataalamu na vifaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali za Zanzibar na wamepanua wigo kwa kuongeza fedha kuwezesha operesheni za figo kufanyika kabla ya mwaka 2020.
Hata hivyo, hakueleza ni kiasi gani cha fedha walichoongeza. Katika sekta ya afya, pia wamekubali kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa nchini hasa ikizingatiwa kuwa Misri ni moja kati ya nchi zenye viwango vikubwa vya ubora wa dawa duniani na hivyo ujenzi huo utaongeza ajira, afya, mapato na kukuza uchumi zaidi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, uwekezaji wa kampuni za Misri nchini ni wa Dola za Marekani milioni 887.07 na umewezesha ajira nyingi.
Kuhusu utalii, Magufuli alisema wamekubaliana kuendesha sekta hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Ndege la Misri na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Kwa sasa Misri inapokea zaidi ya watalii milioni 10 kwa mwaka na Tanzania ni wastani wa watalii milioni mbili kwa mwaka.
Ulinzi ni eneo jingine ambalo marais hao wawili wamekubaliana ili kuhakikisha amani kwa mataifa hayo inaimarika na Rais Al Sisi aliipongeza Tanzania inavyoshiriki kurejesha amani katika nchi za maziwa makuu na Rais Mtaafu Benjamini Mkapa kwa namna anavyosimamia amani Burundi.
Aidha, Tanzania pia itanufaika katika sekta ya elimu, ambapo marais hao wawili wamekubaliana kubadilishana walimu kwa lugha (Kiswahili, Kiarabu na dini) pamoja na IT.
Hata hivyo, pamoja na makubaliano hayo, Dk Magufuli alisema eneo la Mto Nile bado mazungumzo yanaendelea ili kuhakikisha kuwa maji ya Mto huo yanazinufaisha nchi zote zinazoguswa nao.
“Tunatambua maji ya Mto Nile ndio uhai wa Misri, tunatendelea katika mazungumzo ili mto huo umnufaishe kila nchi husika,” alisema Dk Magufuli.
Alieleza pia kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alipata nafasi ya kuongeza na Rais Al Sisi na kueleza changamoto kadhaa za Zanzibar na amekubali kuja tena nchini ili kufanya ziara Zanzibar ambako aliwahi kufika kibinafsi miaka 10 iliyopita.
Eneo jingine marais hao wamesaini makubaliano ya kupambana na rushwa na katika eneo hilo, Rais Magufuli alisema rushwa ni saratani inayohitaji nguvu ya pamoja kuimaliza huku Rais Al Sisi akiisifu Tanzania na Magufuli kwa namna wanavyopambana na rushwa na ufisadi na kueleza ataendeleza ushirikiano katika mapambano hayo.
Rais Al Sisi pia alieleza kuhusu makubaliano hayo na kusisitiza kuwa, Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mikubwa ya maji kwa kujenga visima na kilimo cha umwagiliaji pamoja na maeneo ya afya.
“Namshukuru kaka yangu Rais Magufuli kwa makaribisho mazuri, ili ushirikiano uendelee namkaribisha Misri ili kuendelea kujadiliana namna ya kukuza maendeleo ya nchi zetu,” alisema Field Marshal Al Sisi.
Rais Magufuli alieleza kukubali kuitembelea Misri kwa wakati muafaka.