Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAPACHA WALIOUNGANA WAFARIKI DUNIA

Pacha walioungana ambao walikuwa wakitumia pamoja baadhi ya viungo vya ndani, wamefariki dunia juzi jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa na umri wa siku 26.


Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto wa hospitali hiyo, Zaituni Bokhari alisema jana kuwa watoto hao wamefariki dunia baada ya kupata maambukizi ya kifua kwa muda mfupi.


Alisema kutokana na hali waliyokuwa nayo ilikuwa ni rahisi kwao kupata maambukizi mbalimbali hasa kwenye mapafu na katika baadhi ya viungo vyao.


“Walikuwa wanaendelea vizuri sana ila (juzi) jana ndiyo walibadilika ghafla, wakaanza kuonekana wanapata tatizo la kupumua, hata hivyo, mmoja alizaliwa na tatizo la kupumua,” alisema Dk Bokhari.


Watoto hao walizaliwa katika Hospitali ya Misheni ya Berega, Morogoro, Julai 21.


Kutokana na hali zao, Julai 24 walifikishwa Muhimbili ambako walichukuliwa vipimo mbalimbali vya kuchunguza afya zao na kuangalia uwezekano wa kuwatenganisha.


Baada ya kufanyiwa vipimo vya kimaabara kwa takribani wiki nzima, iligundulika kuwa wanatumia pamoja baadhi ya viungo vya ndani ikiwamo moyo na ini.


Majibu hayo yalikuja baada ya vipimo vya radiolojia vikiwamo CT Scan, MRI, X Ray, moyo (ECO) pamoja na vipimo vyote vya damu.


Mbali ya kugundulika kuwa wanatumia pamoja baadhi ya viungo vya ndani ikiwamo moyo na ini, Dk Bokhari alisema watoto hao wameungana sehemu ya kifua na tumbo na baada ya vipimo vya CT Scan, ikaonekana pia kwamba kuna baadhi ya ogani zimeshikana.


Pia alisema majibu hayo ya CT Scan ya tumbo na kifua yalionyesha kuwa kuna chemba nyingi za milango ambazo walikuwa wakishirikiana.


Pamoja na hali hiyo, Dk Bokhari alisema jopo la madaktari lilikuwa limejiandaa kuwatenganisha watoto hao na kwamba kazi hiyo ilikuwa ifanyike katika miezi sita ijayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com