Mawakili kutoka nje ya nchi wanaomtetea bilionea wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Singh Sethi, kuhusu kupewa dhamana, jana walikwamisha usikilizwaji wa maombi hayo.
Bilionea huyo na mwenzake James Rugemalira, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kuchota mabilioni ya fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), isivyo halali.
Pia, wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo ni miongoni mwa mashtaka yasiyo na dhamana, lakini washtakiwa, kila mmoja kwa wakati wake wameamua kusaka dhamana katika Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka amemuwekea pingamizi bilionea huyo katika maombi yake hayo, ambalo lilipangwa kusikilizwa jana na Jaji Winfrida Korosso, lakini usikilizwaji wa pingamizi hilo ulikwama baada ya bilionea huyo kuamua kuyaondoa mahakamani maombi hayo.
Seth aliamau kuyaondoa mahakamani maombi hayo kutokana na kuhusisha mawakili kutoka nchini Afrika Kusini, ambao aliwakodi kuongeza nguvu kwa kushirikiana na mawakili wazawa kumpigania katika dhamana yake hiyo.
Maombi ya kuyaondoa maombi hayo mahakamani yalitolewa na kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea bilionea huyo, Melkizedeck Lutema, baada ya kubainika mawakili hao wa nje hawakuwa na sifa za kufanya kazi nchini.
Ingawa mawakili hao walikuwa hawajatambulishwa mahakamani, lakini katika nyaraka mbalimbali zinazohusiana na maombi hayo, wametajwa kuwa miongoni mwa mawakili wake.
Kutokana na kasoro hiyo Wakili Lutema aliiomba mahakama iyaondoe maombi hayo kwa lengo la kuanza upya mchakato wa kuyawasilisha mombi ambalo mahakama iliridhia.
Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango, alisema mawakili hao hawana cheti cha kufanya kazi katika mahakama za hapa nchini kutoka kwa Jaji Mkuu.
Wakili Mango alisema kuwa ili wakili kutoka nje ya nchi aruhusiwe kufanya kazi katika mahakama za ndani ni lazima aombe kibali kutoka kwa Jaji Mkuu ambacho analazimika pia kukilipia, jambo ambalo mawakili hao hawakuwa wamelifanya.
Seth na Rugemalira wanakabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye jumla ya mashtaka 12 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa mujibu wa sheria za Tanzania mashtaka hayo hayana dhamana na hadi sasa washtakiwa wanasota mahabusu.