Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Mjumbe wa Kamati Kuu Edward Lowassa wametoa pongezi kwa Rais Mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta kwa kuchaguliwa tena kuongoza nchi ya Kenya kwa awamu ya pili.
Mbowe amewapongeza wananchi wa Kenya kwa kuweza kufanya uchaguzi wa uwazi na haki
"Kwa niaba ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na wapenda Demokrasia wa Tanzania, natoa pongezi kwa chama cha Jubilee na Uhuru Kenyatta kwa kuchaguliwa tena kuiongoza nchi ya Kenya.Lakini pia nawapongeza zaidi wananchi wa Kenya kwa uchaguzi wa uwazi na haki, Mungu ibariki Jumuiya ya Afrika Mashariki" alisema Mbowe
Aidha Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Mhe, Edward Lowassa pia amempa neno Rais Mteule wa Kenya na kusema kuwa ushindi huo wa pili wa Uhuru Kenyatta ni kwamba wananchi wa Kenya wamezungumza kupitia kura kuwa wana imani na uongozi wake na maono yake katika nchi hiyo.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilikuwa kinamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta katika kampeni mbalimbali na kiliweka wazi uhusiano huo kwa kile kilichodai kuwa Uhuru Kenyatta ni mtu ambaye anasimamia Demokrasia.
Social Plugin