Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

METL KILIMO YAMKABIDHI SARUJI MIFUKO 200 MBUNGE WA JIMBO LA KOROGWE VIJIJINI MAJI MAREFU



KAMPUNI ya METL Kilimo imetoa msaada wa mifuko 200 ya Saruji kwa Mbunge wa Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani almaarufu Profesa Majimarefu lengo likiwa kumwezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii hatua ambayo itasaidia kuboresha miundombinu kwa sekta mbalimbali.

Makabidhiano ya msaada huo yamefanyika juzi wilayani Korogwe kati ya mwakilishi wa kampuni ya METL Kilimo,Mtegwa Katuga ambaye ni Meneja ufundi na Mbunge Stephen Ngonyani hatua ambayo imeonekana kuwa ni sehemu ya mchango wa wadau kuharakisha shughuli za kimaendeleo kwa jamii.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo wa tani kumi za Saruji,mbunge Ngonyani alisema Saruji hiyo imekuja kipindi muafaka na itasaidia kukamilisha miradi iliyoanza kutekelezwa kwenye jimbo lake huku akitanabaisha kuwa kipaumbele cha ugawaji saruji hiyo ni kwa wale walioanza kutekeleza miradi.

Aidha aliishukuru kampuni ya METL Kilimo kupitia Rais wake Mohammed Dewji kwa kumpatia msaada huo ambao utakaosaidia kusukuma jitihada za maendeleo katika jimbo la Korogwe vijijini.

“Kwa kweli sikutarajia kupata msaada huu kwa wakati huu,Mungu ambariki huyu rafiki yangu Moo..kweli nilimuomba kwa kumueleza shida yangu akasema atanipa na bila kujua ni lini, leo napigiwa simu kuambiwa nije kupokea Saruji hapa kama mnavyoona Lorry linateremsha”,alisema mbunge Maji marefu.

Mbali na kueleza kuwa kipaumbele cha saruji hiyo kitakuwa kwa
wananchi waliopo maeneo ambayo yameanza kutekeleza miradi hususani ile ya sekta ya elimu, lakini pia Majimarefu alisema kwamba miradi mingine ikiwemo ile ya afya itaangaliwa sanjari na mwananchi mmojammoja pale itakapobidi atasaidiwa..

Aliongeza kuwa  pindi Saruji hiyo
itakapoanza kugawanywa kwenye miradi ya ujenzi, atahakikisha inatumika kama ilivyokusudiwa hatua ambayo itawezesha tija kupatikana na hivyo wananchi kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao.

Naye mwakilishi wa Rais wa METL Mtega Katuga alisema msaada huo ni sehemu ya kampuni katika kusaidia huduma za jamii hatua itakayosaidia kuleta ustawi kwa umma wa watanzania walio wengi.

Katuga alisema licha ya METL Kilimo kutoa msaada huo kupitia mashamba yaliopo yake ya Korogwe huo hautakuwa mwisho kwao kuisaidia jamii huku akiahidi kuendelea kufanya hivyo kila watakapokuwa wakihitjika kusaidia huku akitanabaisha kuwa utaratibu huo unasaidia kuimarisha mahusiano.

Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com