Jeshi la Polisi Dodoma linawashikilia watu 11 kwa uchunguzi kutokana na mauaji ambapo Agosti 8, 2017 majira ya saa 4:00 usiku katika kitongoji cha Chang’ombe Wilaya ya Chamwino mtu mmoja mwanamke aliyefahamika kwa jina la Mariam Saidi miaka 17 mkazi wa Kigoma aliuawa kwa kukatwa shingo na kutenganishwa na kiwiliwili na kuchomwa moto.
Mwili wa marehemu ulikutwa nyumbani kwa mganga wa jadi aitwaye Ashura Mkanga mwenye miaka 33 na mkazi wa kitongoji cha Chang’ombe.
Inaelezwa kuwa mazingira ya tukio yanaonesha kuwa mganga huyo wa jadi asiye na kibali kuendesha shughuli za tiba asili analaza wagonjwa nyumbani kwake, anafanya matambiko, anapiga ramli chonganishi, anafanya tohara za watoto katika nyumba yake pamoja na matambiko.
“Tukio hili ni baya na halikubaliki hapa Dodoma na mahala popote, ni fedheha kubwa sana kwa wananchi kuendelea kukumbatia imani za kishirikina katika karne hii na serikali imesogeza huduma za afya karibu na jamii lakini bado wapo watu hawataki kwenda hospitali na kukubali kuuawa kwa fedheha na waganga wachonganishi”, alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Lazaro Mambosasa wakati akiongea na waandishi wa habari
Social Plugin