Mmiliki wa MALUNDE1 BLOG ambaye ni mwenyekiti wa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Kadama Malunde amekamatwa na jeshi la polisi alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya uandishi wa habari kwenye tukio la wananchi kufunga barabara mjini Shinyanga.
Tukio hilo limetokea leo asubuhi majira ya saa tano katika mtaa wa Magadula Ngokolo Manispaa ya Shinyanga ambapo wananchi waliamua kufunga kwa mawe na matofali barabara inayotoka hospitali ya rufaa mkoani Shinyanga kuelekea gereji ya Mohamed Trans, kutokana na kuchoshwa na vumbi kali linalotokea pindi magari yanapopita katika barabara hiyo.
Vumbi hilo kali linatokana na ujenzi wa muda mrefu wa barabara hiyo ambapo miezi sita iliyopita mkandarasi JASCO alichanganya mchanga na simenti na kumwaga katika barabara hiyo kisha kuitelekeza na hivyo kusababisha vumbi kali kupita linaloathiri shughuli na afya za wakazi wa eneo hilo.
Inaelezwa kuwa Malunde amekatwa na askari polisi wakiongozwa na mkuu wa polisi wilaya ya Shinyanga ambao walimkataza kupiga picha za tukio hilo.