MWANAMKE aliyepigwa risasi na polisi wa jijini Mwanza saa 5:00 usiku wa Jumanne akiwa nyumbani kwake, amesimulia askari hao walivyofikia kumvua nguo.
Akizungumza na Nipashe katika Hospitali ya Rufani ya Bugando jana, Editha Malima (Esther Ntobi), alisema kabla ya mkasa wa kupigwa risasi, yeye na familia yake walikuwa wakila chakula cha usiku huku wakiangalia taarifa ya habari kwenye televisheni.
Alisema ghafla walisikia kishindo nje ya nyumba na baada ya kutoka walikuta gari aina ya Toyota Hiace likiwa limegonga nyumba yao.
“Baada ya kuona nyumba yetu imegongwa, mume wangu alipiga simu Polisi na muda si mrefu askari walifika," alisema Editha.
"Mimi niliingia ndani, lakini muda kidogo nilisikia mume wangu akilia 'mnaniua jamani, nisaidieni'."
"Nilitoka nje nikaona askari saba wanampiga... nilienda kuwaomba msamaha, lakini na mimi walinipiga hadi wakanivua nguo nikabaki uchi wa mnyama.
"Nilifanikiwa kukimbia ndani na mume wangu, lakini walitufuata wakaanza kuwapiga na watoto.
"Niliwaomba wasiwapige watoto, lakini askari mmoja alimwambia mwenzie mpige risasi, nililia nikiomba msamaha ndipo huyu mwingine alinipiga risasi ya mguu na mwingine akanipiga na kitako cha bunduki kidevuni."
Editha alisema askari hao walipompakia kwenye gari la polisi waliendelea kumpiga na kumfikisha kituoni huku damu zikiendelea kuvuja.
Alisema walipofika kituoni walimkalisha chini kwa vipigo ndipo Mkuu wa Kituo (OCS) cha Mabatini aliwakataza.
"Aliwaambia 'msimpige huyu mama, hana kosa lolote'," alisema.
"Niliandikiwa RB na kwenda hospitali (ya mkoa) ya Sekou Toure, lakini ilishindikana, nilihamishiwa Hospitali (ya Rufani) ya Bugando ambayo mpaka sasa naendelea na matibabu.”
DAKTARI BINGWA
Daktari bingwa wa mifupa katika Hospitali ya Rufani ya Bugando, Izidoriy Ngaiyomela amethibitisha Editha kupokelewa hospitalini hapo Agosti 9 majira ya saa 10:30 jioni akiwa na jeraha la risasi katika mguu wake wa kulia.
Aidha, muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, Leokadia Ngovongo alisema majeruhi huyo anaendelea vizuri na matibabu yake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna Ahmad Msangi aliwaambia waandishi wa habari juzi, kuwa amewasimamisha kazi askari wanne wa Kituo Kikuu cha Nyamagana kwa tuhuma za kufyatua risasi ovyo na kumjeruhi mke wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo, eneo la Mabatini.
Kamanda Msangi alisema askari hao ambao hakutaja majina yao, hawakutumwa na jeshi lake kufanya tukio hilo.
Alisema endapo itathibitika kuwa walifyatua risasi hizo kwa makusudi au uzembe, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
Source: Nipashe