Chindika Pingwa, mzazi aliyecharazwa viboko na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga, amedai kushonwa nyuzi tisa kutokana na kipigo hicho.
Odunga alimcharaza viboko Pingwa mwenye umri wa miaka 56 baada ya gari lake kupigwa mawe na watoto wanne, wawili wakiwa ni wa mzazi huyo.
Tukio hilo lilitokea Agosti 11 katika barabara ya Kondoa-Dodoma, kwenye Kijiji cha Paranga wilayani Chemba ambapo gari la Mkuu wa Wilaya huyo lenye namba za usajili STL 669 lilipigwa mawe na watoto na kusababisha kioo cha nyuma kuvunjika.
Katika mahojiano na mwandishi wa habari hii mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani Chemba, Chindika alisema amesikitishwa na kitendo kilichofanywa dhidi yake na kiongozi huyo wa serikali.
Alisema hakuona sababu za kupigwa kwa makosa yaliyofanywa na watoto, ilhali tayari alikuwa mikononi mwa polisi.
Chindika alisema kipigo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya huyo kimemsababishia majeraha kwenye mkononi na kichwa ambapo alilazimika kushonwa nyuzi tisa.
"DC (Mkuu wa Wilaya) alikuwa ananipiga kwa fimbo kubwa. Baadhi ya maeneo ya mwili hasa mikononi yamevimba kutokana na kipigo, wakati ananipiga nilikuwa najaribu kujizuia," alisema.
Alisema zaidi: "Mkuu wa wilaya amenisababishia maumivu makali na alikuwa akinipiga huku nikiwa nimefungwa pingu tayari kupelekwa katika kituo cha polisi Chemba (kipo jirani na Kitongoji cha Morongia, Kijiji cha Kambianyasa).
"Kosa lilifanywa na mtoto mdogo ambaye naye alikimbia, lakini pia wenzake aliokuwa nao walikamatwa na kupigwa, ili waseme mwenzao aliyefanya kosa hilo amejificha wapi."
Chindika aliiomba serikali kuwapa onyo viongozi wanaojichukulia sheria mikononi kupiga raia wasiokuwa na hatia, ili kuepuka kujenga uadui kati yao na wananchi wanaowaongoza.
"Serikali pia, iliangalie suala hili kwa kina kwa sababu linaweza kusababisha maafa kwa wanakijiji na raia wasio na makosa kutokana na baadhi ya viongozi kujichukulia sheria mkononi," alisema zaidi Pingwa.
"Mimi sielewi kitu gani kinaendelea dhidi ya kiongozi huyu wa serikali."
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Morongia, Marius Roman, akizungumza kuhusu tukio hilo, alisema amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Wilaya huyo.
Alisema masikitiko yake yanatokana na ukweli kuwa hakukuwa na sababu ya kiongozi huyo kumpiga Pingwa, ilhali hatua za kisheria dhidi yake zilikuwa zimeshaanza kuchukulia kwa kufungwa pingu na kuingizwa kwenye gari la polisi.
"Kitendo hiki hakijawafurahisha wakazi wa eneo hili," alisema Roman. "Huu ni udhalilishaji na uonevu dhidi ya wananchi."
Mwenyekiti huyo alisema kuna haja ya mkuu wa wilaya huyo, kwenda katika kitongoji hicho na kuomba radhi wakazi wa eneo hilo kwa kitendo alichofanya.
"Licha ya ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Chemba kusaidia kulipa gharama za matibabu na usafishaji wa vidonda vya Chindika, bado haitoshi," alisema mwenyekiti huyo.
"Kinachopaswa ni mkuu huyo, kurejea kuongea na wananchi wa eneo hili na kuomba radhi."