Picha: UKWELI KUHUSU MADINI YA DHAHABU KUGUNDULIWA MJINI KAHAMA... DC AZUIA WANANCHI WASICHIMBE


SERIKALI wilayani Kahama mkoani Shinyanga imepiga marufuku uchimbaji wa madini katika eneo la Shunu kata ya Nyahanga wilayani humo kufuatia kuibuka kwa tetesi jana kuwa eneo hilo lina madini ya dhahabu.

Hayo yamebainishwa leo na mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu wakati akiongea na Kahama Fm kuhusu hatua waliofikia kufuatia wananchi kuingia katika eneo hilo na kuanza kuchimba dhahabu pasipo kuwa na kibali.

Nkurlu amesema kuwa hakuna ruhusa kwa mtu yeyote kuchimba dhahabu katika eneo hilo na ameliagiza jeshi la Polisi kumkamata yeyote atakayepatikana anafanya shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.

Sambamba na hayo Nkulu ameongeza kuwa uchimbaji wa madini una sheria zake hivyo kama mtu anataka kuchimba akate kibali katika ofisi za madini na afuate taratibu zote ikiwa ni pamoja na kuwahamisha wakazi wa maeneo hayo na kuwalipa fidia.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyahanga Maiko Magile amesema kuwa siku ya leo watu siyo wengi kama ilivyokuwa jana na kwamba wanaanza kupungua kutokana na kukosa dhahabu.

Magile ameongeza kuwa kwa sasa kuna uharibifu na uchafuzi mkubwa wa mazingira uliosababishwa na uchimbaji wa Mashimo sambamba na watu kujisaidia ovyo katika eneo hilo kutokana na kutokuwa na vyoo.
Wananchi wakiwa katika eneo ambalo linadaiwa kuwa na dhahabu Shunu Nyahanga Kahama
Wananchi wakiwa eneo la tukio
Wananchi wakichungulia shimo linalodaiwa kuwa na dhahabu
Wananchi wakichimba mchanga
Mzee akiwa na vifurushi vya mchanga
Wananchi wakiendelea kufurika eneo hilo
Askari polisi akiwazuia wananchi wasiingie katika eneo hilo
Wananchi wakimsikiliza kwa makini askari polisi huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post