WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali italipa madeni yote ya watumishi ambayo yamehakikiwa na kukutwa kuwa ni halali.
“Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli alisitisha malipo sababu ya zoezi la kubaini watumishi hewa, sasa kazi hiyo imeshakamilika, yale yaliyobainika kuwa ni halali yatalipwa. Tunataka watumishi mfanye kazi ya kuwahudumia wananchi kwa bidii,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Agosti 12, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliofanyika kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora.
Akiwa katika wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui, Waziri Mkuu alielezwa na baadhi ya wabunge wa mkoa huo kwamba kuna watumishi ambao walihamishwa kutoka manispaa kwenda wilaya za jirani lakini hawajalipwa fedha zao kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu ambaye ameweka utaratibu wa kukutana na watumishi wa umma kila anapofanya ziara za kikazi mikoani, aliwaeleza watumishi wa wilaya hizo kwamba Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.
“Hivi sasa tunadhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya watumishi, hakuna madeni ya matibabu, ya likizo au ya masomo. Kila mtumishi anaruhusiwa kujiendeleza, lakini ni lazima kwanza aandike barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuelezea nia yake na akikubaliwa, ndipo aanze kutuma maombi kwenye vyuo. Mtumishi akiamua kuomba chuoni moja kwa moja ndipo alete madai yale, hatapewa chochote kwa sababu ni nje ya utaratibu,” alisema.
Akifafanua utendaji kazi wa mfumo huo, Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa na kwamba unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja ama kustaafu.
Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.
“Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo,” alisema.
“Mimi nimekuwa kwenye utumishi wa umma kwa muda mrefu, sijawahi kuona mtu anaandikiwa barua ya kupandishwa daraja halafu anakataa. Kikubwa ni kwa maafisa utumishi kuona kama kuna watumishi wanastahili kupandishwa madaraja, watume taarifa zao mapema (kabla ya tarehe 10 ya kila mwezi ili waingizwe kwenye mfumo huu, kisha wawaandikie barua za kuwajulisha wahusika. Hata barua ikichelewa kumfikia mtumishi, mshahara wake hautachelewa na kwa njia hii tutaepuka kuweka madeni yasiyo na tija,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao na akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake.
“Napenda kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuimarisha utendaji wa watumishi lakini pia Serikali hii haitamvumilia mtu mdanganyifu, mzembe, asiye mwadilifu na mla rushwa. Tukikukamata hatuundi tume kwa sababu tume nazo zinamaliza fedha tu. Tukiwa na ushahidi wa kutosha, tunamalizana hapohapo,” aliongeza.