Idara ya Uhamiaji inapenda kuufahamisha Umma kwamba, utolewaji wa pasipoti zenye hadhi ya Kidiplomasia (Diplomatic Passport) na Kiutumishi (Service Passport) upo kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria Sura ya 42 ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni zake.
Katika Vifungu Namba 10(2) na (3) na Jedwali la Pili na la Tatu la Sheria hiyo, makundi mbalimbali ya watu wanaostahiki kupewa pasipoti hizo yameainishwa.
Hivyo, Idara ya Uhamiaji inawataka wale wote ambao wamefikia ukomo wa Utumishi wa nyadhifa na hadhi hizo, warejeshe pasipoti hizo kwenye Ofisi za Uhamiaji ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu tarehe ya kutolewa kwa taarifa hii, kama yalivyo matakwa ya Kifungu cha 8(2) cha Sheria tajwa hapo juu; isipokuwa wale ambao kwa mujibu wa nyadhifa zao wanaruhusiwa kisheria kuendelea kutumia Pasipoti hizo hata baada ya kustaafu kwao wakiwemo Viongozi Wakuu wa Nchi wastaafu, Wakuu wa Mihimili ya dola Wastaafu na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Wastaafu kama ilivyoainishwa katika Jedwali la Tatu kwenye Sheria hiyo.
Baada ya kuisha kwa kipindi tajwa yaani mwezi mmoja baada ya kutolewa kwa taarifa hii, wasiostahiki kuwa nazo watazuiliwa safari zao mara watakapopita katika vituo vya kuingia na kutoka nchini ikiwa ni pamoja na Viwanja vya Ndege. Aidha, ieleweke kwamba, kuendelea kuwa na Pasipoti hizo kwa wasiostahiki ni kosa kisheria chini ya kifungu cha 19(2)(k) cha Sheria tajwa.
Imetolewa na
KITENGO CHA UHUSIANO,
IDARA YA UHAMIAJI,
MAKAO MAKUU.
15 AGOSTI, 2017.
Social Plugin