Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UHURU KENYATTA AENDELEA KUONGOZA MATOKEO YA UCHAGUZI WA RAIS KENYA


Wakati mchakato wa kuhesabu kura za Urais ukiendelea nchini Kenya, kwa mujibu wa matokeo ya awali Rais Uhuru Kenyatta anaonekana kuongoza dhidi ya mshindani wake mkubwa, Raila Odinga anayeungwa mkono na ngome ya NASA.


Hadi majira ya saa mbili asubuhi hii, matokeo ya kura zilizohesabiwa yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya, Kenyatta anaongoza akiwa na asilimia 54.57 (kura 7,546,262) huku Odinga akiwa na asilimia 44.58 (kura 6,164,403 ).


Aidha, Kenyatta anaonekana kupenya katika ngome za Odinga ambapo amefanikiwa kupata zaidi ya asilimia 46 katika jiji la Nairobi ambako ni ngome kuu ya Odinga. Matokeo hayo ya Nairobi ni mafanikio kwa Kenyatta ambaye alipata asilimia ndogo zaidi katika uchaguzi wa mwaka 2013.


Hata hivyo, bado kuna ngome nyingi za Odinga ambazo zinaonekana zinaweza kubadili matokeo kwa kuzipandisha asilimia zake kadiri itakavyowezekana. Katika eneo la Kwale, Odinga amepata asilimia 75 na eneo Kilifi akipata asilimia 83 ya kura.


Kenyatta anaonekana kufanya vizuri maeneo ya Kiambu akiwa na asilimia 93 huku Odinga na asilimia 7, na Kiring’anya akiwa na asilimia zaidi ya 98 wakati kura zikiendelea kuhesabiwa.


Maeneo ambayo wawili hao wameonekana kupambana ni pamoja na Lamu ambapo Odinga amepata asilimia 50 na Kenyatta amepata asilimia 49 wakati kura zikiendelea kuhesabiwa.


Haya ni matokeo ya awali ya vituo takribani 5,400 kati ya 40,883. Wapiga kura waliojiandikisha ni milioni 19,611,423.


Mchakato wa kuhesabu kura unaendelea kwa uwazi na waandishi wa habari wameruhusiwa kuingia ndani ya vyumba vya kuhesabia kura kushuhudia zoezi hilo linavyoendelea majimboni na kurusha moja kwa moja.


Wakenya walipiga kura jana, Agosti 8 na wanatarajia kuyapata matokeo ya uchaguzi huo mapema wiki hiii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com