Uhuru Kenyatta, baada ya kutangazwa mshindi, ametoa wito kwa wananchi kudumisha umoja
Tume ya taifa ya uchaguzi Kenya imemtangaza Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne.
Rais Kenyatta alipata kura 8, 203, 290.. ambayo ni asilimia 54 naye mpinzani wake mkuu, mgombea wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance Raila Odinga akapata kura milioni 6,762,224 ambayo ni asilimia 44.
Akitangaza matokeo hayo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC Wafula Chebukati alisema kuwa ni asilimia 78 ya wapiga kura milioni 19 waliosajiliwa pekee walioshiriki katika shuguhuli hiyo ya kidemokrasia.
Alisema kuwa licha ya matatizo machache kukumba mfumo mpya wa kutangazia matokeo, tume yake ilifanikiwa kutangaza matokeo hayo bila tashwishi yoyote.
Wafuasi wa Jubilee wakisherekea
Aliongezea kuwa hatua zilizochukuliwa kuandaa uchaguzi huo ni hakikisho tosha la ukomavu wa kidemokrasia nchini.
Alisema kuwa Wakenya wengi walijitokeza na kuvumilia hali ya anga ili kushiriki katika zoezi hilo la kidemokrasia kutokana na uaminifu walio nao kwa tume hiyo ya uchaguzi.
Aliongezea kwamba licha ya kukumbwa na changamoto chungu nzima katika mahakama waliweza kuandaa uchaguzi huo kwa njia ya haki uwazi na uhuru,
Akitoa hotuba yake rais Uhuru Kenyatta amewashukuru wafuasi wake na Wakenya wote kwa jumla kwa kumpatia muhula mwengine.
Aidha amemtaka mpinzani wake mkuu Raila Odinga na wafuasi wake kushirikiana naye katika kujenga Kenya akisema kuwa Uchaguzi huja na kumalizika lakini wakenya ni sharti wasalie kama mandugu na majirani wema.
''Katika kila mashindano kuna mshindi na aliyeshindwa ,hivyobasi namuomba ndugu yangu mkubwa Raila Odinga na wafuasi wake kushirikiana nami katika kulijenga taifa hili kwa sababu uchaguzi huja na kumalizika lakini wakenya ni sharti wanedlea kuwa majirani wema'', alisema Uhuru Kenyatta .
Na muda mfupi tu baada ya Uhuru Kenyatta kutanzwa rais mteule wafuasi wake kote nchini walisherehekea ushindi huo kwa vifijo na nderemo.
Muungano wa upinzani ulikuwa umepinga utaratibu uliokuwa unatumiwa na tume hiyo kupeperusha matokeo ya uchaguzi huo.
Aidha, viongozi wa muungano huo walikuwa wamedai mitambo ya tume hiyo ilidukuliwa na matokeo kubadilishwa.
Viongozi hao walikuwa Alhamisi wametangaza kwamba mgombea wao, Bw Odinga ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu katika serikali ya Mwai Kibaki, kuwa mshindi wa uchaguzi huo.
Social Plugin