Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI 22 WA MILAMBO SEKONDARI WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Wanafunzi 22 wa Shule ya Sekondari ya Milambo ya mkoani Tabora wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka 12 matano yakiwa ya kujeruhi na saba ya kuharibu mali, ambapo mmoja amesomewa tuhuma zake akiwa amelazwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete.


Upande wa serikali ukiongozwa na wakili Iddy Mgeni ulidai mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Tabora, Emanuel Ngingwana kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo 12 Agosti 14 mwaka huu majira ya usiku.


Wakili Mgeni alidai katika mashitaka ya kwanza hadi ya tano kuwa siku hiyo, watuhumiwa kwa pamoja waliwashambulia na kuwajeruhi wakazi watano wa kata ya Chemchem kinyume na kifungu namba 241 sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.


Aliwataja walioshambuliwa na kujeruhiwa kuwa ni Juma Farahani, Iman Elias, Salehe Ally na Ahmed Haruna wakazi wa mtaa wa Uhuru na Hamza Jafary mkazi wa mtaa wa Dawa.


Katika mashitaka ya sita na saba, walidaiwa siku hiyo watuhumiwa kwa pamoja waliharibu mali ya Shaban Farahani chini ya kifungu namba 326 (1) cha sheria ya makosa ya jinai huku wakijua kwamba ni kosa.


Upande wa mashitaka ulidai katika mashitaka ya nane kuwa watuhumiwa waliharibu vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh 440,000 zikiwemo spika mbili, dirisha moja na simu mbili mali ya Hemed Rajab.


Wanafunzi wa sekondari ya Milambo wanatuhumiwa kuvamia nyumba ya kulala wageni iitwayo Nyakitonto na kuharibu taa tano na bango vyote vikiwa na thamani ya Sh 750,000 mali ya Asia Maulid wakati katika shitaka la 10 ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao waliharibu turubai mbili, milango miwili, sahani na vikombe, dirisha mbili, juzuu boksi tatu zinazotumiwa na waumini wa dini ya kiislam mali ya Ally Juma, yote ikiwa na thamani ya Sh 4,278,000.


Watuhumiwa wote walikana na mahakama ilisema dhamana ipo wazi na walitakiwa wadhamini wawili kwa kila mtuhumiwa mmoja ambao watasaini mkataba wa ahadi ya Sh milioni mbili kila mmoja na shauri hilo limeahirishwa hadi Agosti 31, 2017.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com