Wazazi, watoto na watu mbali mbali wameshindwa kujizuia na kumwaga chozi walipokuwa wakiwapokea watoto Sadia Ismail, Doreen Eribariki na Wilson Tarimo, ambao wamerejea rasmi nchini wakitokea nchini Marekani walikokuwa wakipatiwa matibabu.
Watoto hao ambao ni manusura wa ajali iliyoua takriban wanafunzi 32 wa shule ya msingi Lucky Vicent, wamepokelewa na viongozi mbali mbali wa serikali wakiwemo Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Anna Mghwira, Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu, wazazi na wanafunzi wa shule ya Lucky Vicent, waliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Watu mbali mbali walihudhuria uwanjani hapo wakiwa na mashada ya maua kuwalaki huku kukiwa na burudani mbali mbali kutoka kwa sanii Mercy Masika wa Kenya, Angel Bernad wa Tanzania na Kwaya ya Shangwe kutoka jijini Arusha.
Shirika la Samaritan Purse la Marekani lilijitolea kusaidia watoto hao kuanzia usafiri na gharama za matibabu kwa muda wote ambao walikuwa nchini humo wakitibiwa, katika Hospitali ya Sioux City tangu mwezi Mei 15, kufuatia majeraha makubwa kwenye ajali kubwa waliyoipata tarehe 6 Mei 2017, wakitokea hospitali ya Mt. Meru Arusha.
Social Plugin