WATU 11 wanashikiliwa na Polisi mkoani Dodoma akiwemo mganga wa jadi, Ashura Matha (33), wakituhumiwa kuhusika na kifo cha Mariam Saidi (17) aliyeuawa kikatili kwa kukatwa shingo, kutenganishwa kiwiliwili na kuchomwa moto kichwa na sehemu za mwili wake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa alisema mwili wa Mariam ulikutwa nyumbani kwa mganga huyo wa jadi katika kitongoji cha Chang’ombe Kijiji cha Chamwino-Ikulu wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Kamanda Mambosasa alisema mauaji ya Mariam ambaye ni mwenyeji wa Kigoma, yalifanyika juzi saa nne 4.00 usiku katika kitongoji hicho, ambako wauaji walimkata shingo, wakatenganisha na kiwiliwili, wakachoma moto kichwa na kubakia fuvu lisiloweza kutambuliwa sura yake. Pia baadhi ya sehemu za mwili ukiwamo mkono wa kushoto, shingo, kifua na sehemu za siri ziliunguzwa vibaya.
Alisema mazingira ya tukio hilo mahali lilipotokea, yanaonesha kwamba mganga huyo wa jadi asiye na kibali cha kuendesha shughuli za tiba asili, pia analaza wagonjwa nyumbani kwake, anawafanyia matambiko, anapiga ramli chonganishi na anafanya tohara kwa watoto. “Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi pia linawashikilia watu wanane ambao walikuwa wamelazwa katika nyumba hiyo siku ya tukio wakiwamo wanawake sita na wanaume wawili,” alisema.
Kamanda Mambosasa na kuongeza kuwa waliwakamata watu wengine wawili ambao ni Msaidizi wa mganga wa jadi, Victor Chibelenje (24) ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Mwongozo, Kijiji cha Chamwino na mume wa mganga huyo na Noel Mazengo ambaye ni mkazi wa Chang’ombe, katika kijiji cha Chamwino- Ikulu.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo la kusikitisha na pia kuchunguza namna ambavyo Mariam alifika kijiji hicho kutoka mkoani Kigoma. Kamanda wa Polisi alisema jeshi lake linalaani tukio hilo baya na la kinyama na hakikubaliki mahali popote, ni fedheha kubwa kwa wana-Chamwino kuendelea kukumbatia imani za kushirikina katika karne hii, hasa wakati serikali imesogeza huduma muhimu za afya karibu na maeneo ya jamii.
Alitoa mwito kwa waganga wa jadi wote wanaoendesha ramli chonganishi katika maeneo mbalimbali ya jamii, wafichuliwe ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua kabla hawajaufikisha mkoa katika hatua mbaya na ya fedheha zaidi. Wakati huohuo, mkazi wa Kijiji cha Ntyuka Kata ya Ntyuka katika Manispaa ya Dodoma, Masumbuko Nyerere (24), amekufa kwa kufunikwa na kifusi cha mchanga. Kamanda Mambosasa alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 1.00 asubuhi kijijini hapo katika eneo la machimbo hayo baada ya kufukiwa na kifusi cha mchanga wakati anachimba.
Chanzo-Habarileo
Chanzo-Habarileo