Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATU 32 WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MAUAJI NZEGA

Watu 32 wamefikishwa mahakamani kujibu shtaka la mauaji ya wanawake watano yaliyotokea katika Kijiji cha Undomo Kata ya Uchama wilayani Nzega.


Miongoni mwa waliofikishwa mahakamani jana Jumatatu na kusomewa shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega, Sarafina Nsana wamo viongozi wa serikali ya kijiji hicho na wengine wa ngazi ya kata.


Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Melito Ukongoji aliiambia mahakama kuwa Julai 25, washtakiwa kwa pamoja, wakiwa katika kijiji cha Undomo waliwashambulia kwa kuwapiga na kuwachoma moto hadi kufa wanawake watano kwa tuhuma za imani potofu za ushirikina.


Akisaidizana na mwenzake, Agustino Nshimba mwendesha mashtaka huyo aliwataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni Nsuku Masali, Ester Kaswahili, Christina Saidi, Mwashi Mwinamila pamoja na Kabula Kagito.


Waliosomewa mashtaka ambao hata hivyo hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri ya mauaji ni pamoja na Mtendaji wa Kata ya Uchama, Malewa Maroji, Diwani wa Kata hiyo, Karoli Massanja, Kiongozi wa Sungusungu, Dotto Saraganda, mwenyekiti wa kijiji, Ramadhani Kulwa na mtendaji wake, Rauliani Sanyiwa.


Washtakiwa wengine ni Dotto Saraganda (49), Taus Ngassa (40), Pill Kapewi (25), Leons Sospeter (36), Issah Eliudi (20), Nhungulu Sospeter (25), Saidi Nsabi(25), Emmanuel Pius(18), Estar Muhamila(25), Tatu Thomas (35), Thotunatus Ngelera (30), Milika Daudi (36), Kisuge Ntemi(31), Kulwa Kizinza (40), Shija Masali (35), na Kulwa shomali(31).


Wengine ni Selelo Mashandete (46), Steven Saraganda (60), Paul Christoph (60), Makuya Athumani(42), Peter Mapalala(21), Maganga Daudi (19), Omary Seleli (20), Paul Emmanuel (51),Charles Kiberiti (26), Emmanuel Mihayo (27), Shomali Nhyama (75), pamoja na Shija Shomali (20).


Shauri hilo imeahirishwa hadi Septemba 4, itakapotajwa tena na muda wote wakati washtakiwa wakisomewa mashtaka dhidi yao, jeshi la polisi liliimarisha ulinzi kuzunguka eneo la mahakama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com