Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ASKOFU NIWEMUGIZA : NIPO TAYARI KUITWA MCHOCHEZI


Askofu wa Kanisa Katoliki Ngara, Severin Niwemugizi amesema yuko tayari kuitwa mchochezi endapo kundi la watetezi wa haki za binadamu watachukuliwa kama wachochezi.

Askofu Niwemugiza amesema yeye kama kiongozi wa dini anaongozwa na maadili, haki na ukweli hivyo hajali namna wengine watakavyomchukulia.

Akifungua mkutano wa asasi za kiraia uliolenga kujadili kuhusu Katiba Mpya leo Jumatano, Askofu Niwemugizi amesema imefika wakati nchi inahitaji kuwa na dira nzuri.

Amesema hakuna mtetezi wa haki za binadamu anayetaka nchi iingie kwenye machafuko kwani wote lengo lao ni kuchochea maendeleo, amani na utulivu.

Askofu Niwemugizi amesema kuanza kutokea kwa matukio ya kuteka watoto, vifo katika mazingira ya kutatanisha na ongezeko la watu wasiojulikana ni ishara mbaya.


"Hizi sio dalili nzuri kwa Taifa lenye afya njema. Ni vielelezo vyenye dira mbaya. Imefika wakati tukae kama Taifa tukubaliane kuwa tunataka dira njema ambayo ni Katiba."


Amesema anatambua jitihada anazofanya Rais John Magufuli katika kupambana na ufisadi na kutaka rasilimali ziwanufaishe wanyonge lakini ni muhimu juhudi hizo zilindwe na Katiba nzuri.


"Rais anafanya mengi mazuri na alipoanza kila mmoja aliona dalili za matumaini lakini juhudi hizo zinaweza zisiwe endelevu kama hakuna ulinzi wa Katiba,”


"Tunahitaji Katiba tena Katiba nzuri ambayo haitaruhusu kuchezewa na yeyote kwa maslahi au matakwa yake binafsi."


Amesema, "Namshauri Rais achunguze kwa makini yatakayozungumzwa kwenye mkutano huu, ayaone kuwa yana nia njema na ayafanyie kazi."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com