Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amefunguka na kudai atahakikisha yeye na wabunge wanampa ushirikiano Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyeapishwa leo baada ya kuteuliwa siku ya jana Septemba 10 mwaka huu.
Ndugai ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anatoa salamu za wabunge katika ghafla hiyo ya uapisho iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa bila ya kumsahau Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
"Sisi kama bunge tunawahakikishia ushirikiano mkubwa sana kwa kuhakikisha kazi za Mahakama zinaendelea kama zilivyo kikatiba na tutaheshimu sana. Yale maneno na makombora moja moja ya bungeni ni vitu vya kawaida, ndiyo utamaduni wa bunge",amesema Ndugai.
Aidha, Ndugai amesema Mahakama inamchango mkubwa kwa wananchi pamoja na taifa kwa ujumla kwa kuwa hicho ndicho chombo pekee kinachoweza kumtetea mnyonge kuweza kupata haki yake kutoka kwa waporaji.
"Kuwepo kwa Mahakama ndiyo usalama wetu, amani, kheri na matumaini ya mnyonge katika sheria na maamuzi ya Mahakama. Kwa hiyo tunakutakia kila la kheri katika kazi yako, tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu na tutakusaidia na kuomba msaada wako",amesisitiza Ndugai.
Kwa upande mwingine, Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma ameahidi kufanya kazi katika maadili ya kisheria pamoja na kurudisha imani ya wananchi kuhusiana na kupata misaada ya kisheria inayotolewa katika Mahakama mbalimbali ndani ya Tanzania
Social Plugin