DAKTARI : MANJI ANAWEZA KUPOTEZA MAISHA MUDA WOWOTE

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Hospitali ya Aga Khan, Mustapha Bapumia (62) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anashangaa mtu mwenye umri mdogo kama Yusuf Manji (41) kuwa na vyuma vinne kwenye moyo.


Alieleza kuwa na vyuma vinne kwenye moyo ni hatari na kwamba anatembea katika kamba nyembamba.


“Kitaaluma huyu ni lazima ajiangalie sana yupo katika hatari anaweza kupoteza maisha muda wowote.”


Dk Bapumia ambaye ni shahidi wa tatu wa upande wa utetezi alimeeleza hayo jana Jumatatu mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili Manji ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroine.


Akiongozwa na Wakili Hajra Mungula kutoa ushahidi, Dk Bapumia alisema yeye kwa siku huwa anawaona wagonjwa 50 hadi 60 na kwamba Februari 21, 2017 ilikuwa ni mara ya kwanza Manji kupelekwa kwao akiwa na maumivu ya moyo.


Ameeleza kuwa wana utaratibu wa wagonjwa tete kuwapeleka katika kitengo cha dharura na kwamba Manji walimpokea, wakamlaza, wakamchunguza na kuona ana tatizo sugu la moyo pamoja na kuwa na umri mdogo.


"Nikatafuatilia historia na kubaini licha ya kuzibuliwa kwa mishipa yake mitatu India, Dubai na Marekani, ilikuwa bado haijaziba lakini alikuwa bado anapata maumivu ya moyo," ameeleza shahidi huyo.


Ameeleza kuwa walimfanyia vipimo na vilionyesha tatizo lipo na kuna sehemu ya nne inahitaji kuzibuliwa na kwamba mgonjwa alikuwa wazi kuwa anatumia sigara na pombe.


Kutokana na hali hiyo ameeleza walimshauri mgonjwa ili waweze kuzibuliwa lakini akawaambia waache na akaomba dawa kwa kuwa familia yake ipo Marekani na matibabu yake mengi yanafanyika huko.


Shahidi huyo alieleza kuwa wao kama hospitali hawezi kufanya chochote bila ridhaa ya mgonjwa hivyo wakampatia dawa na akaruhusiwa Februari 24, 2017.


Alieleza kuwa siku hiyo hiyo alirejeshwa tena hospitalini hapo nyakati za saa mbili usiku akisumbuliwa na maumivu kwenye moyo, wakamlaza mpaka tarehe Machi 14, 2017 ambapo aliruhusiwa.


“Katika kipindi hicho Manji aliridhia na kuzibuliwa vyuma kwenye moyo.”


Ameeleza kuwa walimpatia dawa ikiwamo za kupunguza kolestro (mafuta) kupunguza maumivu sugu ya mgongo pamoja na kupunguza hofu ambazo zimo ndani ya Morphine na Benzodiazepines.


Kwa upande wake Manji akijitetea aliiomba Mahakama imuachie huru.


Akitoa ushahidi wake alieleza kuwa yeye ana matatizo ya moyo ya kurithi kutoka kwa babu zake ambao walikwishafariki kwa ugonjwa huo.


Ameeleza kuwa ugonjwa wa moyo ulimuanza akiwa na umri wa miaka 26 na kwamba mara nyingi amekuwa akitibiwa nje ya nchi ikiwamo India na Marekani na ana vyuma vitano kwenye moyo.


Akitoa ushahidi mahakamani hapo, Manji ameeleza kuwa kila baada ya miaka miwili anavibadilisha na kufanya uchunguzi vinafanya kazi vipi.


Akiongozwa na wakili wake, Hajra Mungula, Manji ameeleza kuwa katika ripoti zake za kati ya 2009 na 2016 haijawahi kutokea akaonekana kama anatumia dawa za kulevya.


Manji akiendelea kujitetea ameeleza kuwa anatumia vidonge 30 hadi 35 kwa siku.


Manji ameeleza kuwa polisi walikuwa wastaarabu wanampatia dawa na kwa upande wa Magereza vidonge vilikuwa katika kabati wanampatia.


Manji ameeleza kuwa Februari 8, 2017 alipata taarifa ya kutuhumiwa utumiaji wa dawa za kulevya na kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum (ZCO).


Baada ya kuipata taarifa hiyo ameeleza aliitisha mkutano na waandishi wa habari kukanusha taarifa hiyo na Februari 9, 2017 alikwenda polisi kwa sababu anaheshimu jamuhuri na alitaka kazi ifanyike kwa haraka.


Ameeleza alivyokwenda alichukuliwa na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo alikutana na Gwajima(Askofu Josephat) na akatoa sampuli ya mkojo.


Ameeleza kuwa baada ya hapo walikwenda kukagua nyumbani kwake walichukua kompyuta, credit card na visa card.


Amesema kuwa anashangaa kwanini walichukua hivyo vitu wakati havihusiani na kesi ya dawa za kulevya na kuliacha sanduku lililokuwa na sindano na vifaa tiba.


Aliongeza kuwa inajulikana kuwa kuna ugomvi wa kibiashara ambapo wanagombea kampuni ya Tigo na kwamba hiyo kesi ni propaganda na ni mchezo mchafu.


Amesema hiyo kesi imemuathiri yeye binafsi na baba yake alimuachia vitu viwili jina zuri na maadili kwa jamii.


Pia imemuaribia jina kwa jamii yake, msikitini anashindwa kwenda kusali, biashara pia na imeumiza watoto na imemfanya aachie Uenyekiti wa Klabu ya Yanga.


Amesema kuwa kutokana na kesi hiyo anaona aibu kukaa na viongozi ambao anafahamiana nao akiwamo Raila Odinga na rais mstaafu Benjamin Mkapa


Kesi hiyo imeahirishwa hadi leo itakapoendelea kwa ushahidi wa upande wa utetezi.


Awali Manji alidai kuwa yeye ni mshauri wa kampuni za familia na kwamba alikataa tuhuma za dawa za kulevya ili mahakama imsikilize na kutenda haki na kwamba dawa aina ya Morphine na Benzodiazepines ni sehemu ya dawa zake ambazo anatumia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post