Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

FAMILIA YA TUNDU LISSU KUFANYA KIKAO KIZITO

Shangazi yake Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, Ninaa Sawa(kushoto) akiwa na mama mdogo wa Lissu, Bula Muro nyumbani kwa wazazi wa Mbunge huyo Mahambe, Ikungi Singida. Picha zote na Herieth Makwetta. 
***

Siku 10 baada ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi, familia yake imezungumzia tukio na kusema mwishoni mwa mwezi huu watafanya kikao Dar es Salaam wajue nini cha kufanya.


Baba mdogo wa Lissu, Muro Sawa (79), alisema kitu ambacho wazazi wangefurahia ni kumwona kijana wao akirudi nyumbani akiwa mzima.


“Familia tutakaa kikao kushauriana ili tujue suala hili tunalitatua vipi, lakini niiombe Serikali kumzidishia ulinzi kijana wangu. Sisi familia tuna uchungu mkubwa kuhusu hili,” alisema Sawa.


Shangazi wa Lissu, Ninaa Sawa Muro (83) alisema, “Tunakula chakula hakishuki, matonge yanakaba shingoni, maungo yote yanauma kwa sababu ya mtoto wetu, tangu siku ile niliposikia nilikuwa kwenye kiti ghafla nikaanguka na kuanza kutetemeka.”


Alisema alijisikia vibaya baada ya kuambiwa na mtoto wake taarifa hizo, “Aliniuliza umesikia kwamba Tundu Lissu amepigwa risasi? Nikanyamaza, nikaona joto. Kwa jinsi shangazi yangu anavyonipenda hata anikute Manyoni hata Dar es Salaam ananiita jina langu la kikwetu anakuja ananikumbatia iliniuma sana.”


“Alifanywa hivyo kwa nini? Kama tunavyojiona wote roho moja tumfikirie huyo Tundu Lissu,” alisema shangazi huyo ambaye baada ya baba yake Lissu kuzaliwa ndiye aliyemfuata.


Mama mdogo wa Lissu, Bula Muro, alisema baada ya kupata taarifa alianguka chini na kuanza kulia hakufikiria kama amepona.


Mitandao ilivyoiliza familia


Mmoja wa wanafamilia, Msengi Ntandu Mughwai alisema walipata shida siku hiyo ya tukio, “Tulipanga kwenda Dodoma wakasema turudi anaendelea na matibabu, tulihisi wanatudanganya sababu mtandaoni wanasema hali mbaya na kwa kuwa walikuwa ni wanafamilia waliotushauri, tuliamua kurudi usiku kwa kweli kesho yake kulikuwa na habari za ajabu kwenye mitandao yaani zilituumiza sana,” alisema.


Msengi alisema walikuwa wakipigiwa simu na kupewa taarifa zenye utata na wakiingia mitandaoni wanaona habari za ajabuajabu na kwamba hali kwao ilikuwa mbaya.


“Kwa kweli tulipata shida, wazazi wetu walikuwa wanakuja mara kwa mara tunawajibu kwamba anaendelea vizuri lakini wazee wetu walikuwa wanapata taarifa mbaya kwingine kutokana na mitandao ya kijamii,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com