Kufuatia tukio lililowashtua wengi jana la Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi, Spika wa Bunge, Job Ndugai (Mb) ametoa taarifa kwa ufupi kuhusu tukio hilo kabla ya kuendelea kwa mkutano wa nane wa Bunge mjini Dodoma.
Akimnukuu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Spika Ndugai amesema kuwa, katika tukio la kushambuliwa kwa Mbunge Tundu Lissu, kati ya risasi 28 hadi 32 zilifyatuliwa katika gari lake.
Kuhusu risasi zilizompata Tundu Lissu, Spika amesema kuwa alilengwa na risasi 5. Kati ya risasi hizo, 1 ilimlenga mkononi, 2 zilimpata tumboni na 2 zikamlenga mguuni.
Baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo, amesema kuwa wao kama Bunge tayari walikuwa wameandaa ndege ya kumsafirisha hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu zaidi ambayo ilikuwa uwanjani saa 10 jioni, lakini familia yake ikaomba kwamba apelekwe kutibiwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi.
Akitolea ufafanuzi huo ambao upo nje ya utaratibu wa Bunge, Spika Ndugai alisema kwamba, familia hiyo siyo kwamba hawana imani na hospitali au watalaamu wa Tanzania, lakini walisema wangejisikia faraja kama ndugu yao angetibiwa Nairobi, hivyo wakakubaliana nao.
Kufuatia mabadiliko hayo, ilitafutwa ndege nyingine, ambapo majira ya saa sita za usiku, Tundu Lissu akiwa na mkewe, Daktari Bingwa wa Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, waliondoka Dodoma kuelekea Nairobi kwa ndege ya Flying Doctors ambapo wamewasili salama.
Spika Ndugai amesema kuwa tukio hilo ni la kipekee kuwahi kutokea kwa mbunge kushambuliwa hivyo tena wakati ambapo vikao vya bunge vinaendelea.
Aidha, amewataka wabunge na watu wengine, kutoanza kutoa shutuma kwa upande wowote kwani ni mapema bado, na kuwasihi kuviachia kazi hiyo vyombo vya ulinzi na usalama vilete ripoti iliyo kamili.
Tundu Lissu alishambuliwa jana mchana alipokuwa akitoka bungeni kwenda nyumbani kwake eneo la Area D Dodoma ambapo risasi zilifyatuliwa kuelekea kwenye gari lake na kumsababishia majeraha kadhaa.
Social Plugin