Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto ameeleza kusikitishwa kwao na kitendo cha dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kutokufika polisi na kutoa maelezo yake.
Kamanda Muroto amesema hayo leo Jumatano wakati akijibu swali la upelelezi unaendeleaje kuhusu tukio hilo.
Amesema upepelezi unaendelea kuhusu tukio la Lissu kupigwa risasi na watu mbalimbali wanaendelea kuhojiwa wakiwemo wamiliki nane wa gari aina ya Nissan ambazo zilikamatwa kuhusiana na shambulizi hilo.
“Wamiliki wa gari tumewahoji na tunapogundua hakuna muunganiko wowote basi tunaachana nao maana hakuna haja ya kuendelea kuwashikilia au kushikilia gari hizo,” amesema.
Hata hivyo Kamanda Muroto amesema anasikitishwa na kitendo cha aliyekuwa dereva wa mbunge huyo wakati wa tukio kutoonyesha ushirikiano kwa jeshi la polisi.
“Tunasikia yupo nje ya nchi na hadi leo hajaitikia wito wa kufika polisi kupata maelezo yake ambayo yangesaidia katika upepelezi wa tukio hilo.”
Social Plugin