Katika hali isiyokuwa ya kawaida wagonjwa na watu waliokuwa katika hospitali ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga wamepigwa butwaa baada ya fisi mmoja kuonekana akirandaranda ndani ya eneo la hospitali hiyo iliyopo mjini Kahama.
Tukio hilo limetokea leo Ijumaa Septemba 22,2017 asubuhi.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Dr. Lucas David amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 12 alfajiri ambapo fisi huyo ambaye mpaka sasa haijulikani alitokea wapi, alipoingia ndani ya hospitali hiyo.
Amesema licha ya eneo la Hospitali hiyo kuwa na uzio mkubwa,lakini fisi huyo huenda aliingilia katika chuo cha Manesi ambapo kuna tundu karibu na chumba cha kuhifadhia maiti.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Fredrick Malunde amesema baada ya fisi kuonekana walimuarifu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji ambaye aliwaarifu watu wa Idara ya Maliasili ambao walifanikiwa kumuua fisi huyo kwa kumpiga risasi tatu.
Tukio la fisi huyo linakuja siku moja baada ya taarifa kuwa kundi la fisi limevamia na kukatakata mabomba ya maji ya Mradi wa Kilimo cha Mbogamboga wa kikundi cha Songambele katika kata ya Nyandekwa Halmashauri ya Mji wa Kahama.
Chanzo-Kijukuu blog