Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MHANDISI MGAYA : ASILIMIA 95 YA MIRADI YA KUBORESHA UMEME WA TANESCO DAR ES SALAAM IMEKAMILIKA

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limesema, tayari asilimia 95 ya uboreshaji miradi ya umeme katika jiji la Dar es Salaam, imekamilika.

Meneja Mwandamizi wa TANESCO Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi, Mahende Mgaya, (pichani juu), amewaambia
waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo Septemba 27, 2017 na kwamba ifikapo Desemba mwaka huu wa 2017, wananchi na wakazi wa Dar es Salaam wataona ile hali ya kukatika kwa umeme, mara kwa mara imebadilika.

“Tulikuwa na jumla ya miradi mipya 18 ya kuboresha vituo vya umeme jijini Dar es Salaam ili viweze kutoa umeme wa kutosha na wa uhakika, hadi sasa, vituo vinane vimekamilika kabisa na vinafanya kazi, vimebaki vituo 10 ambavyo navyo viko
katika hatua za mwisho za kukamilika, na ifikapo Desemba, 2017 vituo vyote 18 vitakuwa vinafanya kazi”,alitoa hakikisho Mhandisi Mgaya.

Alisema, kufuatia kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na idadi ya watu jijini Dar es Salaam, mahitaji ya nishati ya umeme nayo yameongezeka na hivyo Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliamua kuchukua hatua za haraka kuboresha vituo vyake vya umeme ikiwa ni pamoja na kujenga vipya ili kukidhi mahitaji halisi ya umeme.

“Wafadhili kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika, (AfDB, World Bank, Finland, na Japan), walijitokeza na kufadhili miradi hiyo”,alifafanua.

Kazi hiyo ya kuboresha vituo hivyo ambavyo ni pamoja na Mbagala, Kurasini, Kigamboni, Ilala Mchikichini, Kisutu, Mikocheni, Gongolamboto, na maeneo mengine imekuwa
ikifanyika tangu miaka miwili iliyopita lakini kutokana na matatizo ya hapa na pale, ikiwa ni pamoja na mapingamizi ya wananchi kuzuia utekelezaji wa miradi hiyo, na wakandarasi, kumepelekea ucheleweshaji.

Maeneo ambayo yamekuwa yakiathirika zaidi na hali hiyo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara ni pamoja na Wilaya ya Temeke, Kigamboni, Ubungo na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Kinondoni.

“Nichukue fursa hii kuwaomba radhi wananchi, hususan wateja wetu, kutokana na hali hii ya kukatika kwa umeme, lakini napenda pia waelewe kuwa hali hiyo inatokana na kazi
ambayo tumekuwa tukiifanya, na mara nyingi umeme tunakata siku za weekend, kwa vile shughuli nyingi za kiofisi zinakuwa zimepungua na hivyo inakuwa fursa
nzuri kwetu kufanya kazi”,alifafanua Mhandisi Mgaya.

Alisema wananchi wanataka umeme, tena ulio bora na wa uhakika, ndiyo maana TANSCO imeamua kuchukua hatua madhubuti za kuboresha na kujenga vituo vipya vya kupoza
na kusambaza umeme ikiwa ni pamoja na kujenga lini mpya za kusafirisha umeme.

“Hatua hizi zote lazima ziwe na changamoto za hapa na pale, lakini kwa kiasi kikubwa TANESCO inaelekea kulitatua tatizo hilo la umeme jijini Dares Salaam na
Mkuranga”,alisisitiza.
Wakandarasi na mafundi wa TANESCO wakiwa kazini
Moja ya vituo ambavyo vimefungwa mitambo mipya ili kuboresha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam.
Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Kisutu.

Picha na K-VIS BLOG/Khalfan Said


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com