Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKE AMCHOMA KISU MMEWE...CHANZO MKE HATAKI KUZUIWA KUFANYA STAREHE

Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Maria Mwanahiya mkazi wa  kijiji cha Ntatumbila  wilaya Nkasi mkoani Rukwa amemjeruhi vibaya mume wake kwa kumchoma kisu ubavuni kwa madai kuwa alipata hasira baada ya kukerwa na kitendo cha mume wake kumlazimisha kuacha starehe zake ikiwemo kunywa pombe.


Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 10:30 usiku katika kijiji cha Ntatumbila  wilaya Nkasi mkoani Rukwa muda mfupi baada ya mwanamke huyo kurejea nyumbani kutoka kilabuni alipokuwa anakunywa pombe. 

Inaelezwa kuwa mwanaume huyo aliporudi nyumbani kwake kutoka katika shughuli zake hakumkuta mke wake na wala mke hakuweka chakula kwa ajili ya mmewe hali iliyomlazimu kumfuata mkewe kwenye kilabu ya pombe.

Alipofika kilabuni, alimlazimsha mkewe kurudi nyumbani lakini mwanamke huyo aligoma,hata hivyo baadhi ya watu waliokuwa wanakunywa naye pombe walimsihi arudi nyumbani, ndipo alipokubali kwa shingo upande akarudi na mmewe.

Baada ya kufika nyumbani ulizuka ugomvi mkubwa wa kurushiana maneno kati ya wanandoa hao ambapo mwanamke huyo alikuwa akimwambia mumewe aache kumfuata fuata anapokuwa kwenye starehe zake  kwani yeye siyo mtumishi wa nyumbani.

Wakati wakiendelea kufokezana kwa muda mrefu, ndipo mwanamke huyo alipoamua kwenda jikoni kuchukua kisu na kumchoma mumewe ubavuni na kumsababishia jeraha kubwa ambalo lilivuja damu nyingi.

Tukio hilo lilisababisha watu kujazana katika nyumba yao na kuamua kumkamata  mwanamke huyo na kumpeleka kituo cha polisi na mume wake  kumkimbiza hospitalini ili akapatiwe matibabu ili kuokoa maisha yake.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Ntatumbila Daniel Kalumbilo ameiambia Malunde1 blog kuwa hilo ni tukio la pili kwa mwanamke huyo kumshambulia  mumewe kwa silaha za jadi ambapo aliwahi kumpiga mpini  na kumuumiza kichwa mpaka akafanyiwa upasuaji.

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwasihi wanandoa kujitahidi kutatua migogoro yao kwa njia ya amani na iwapo wanashindwa wawashirikishe ndugu wengine kuliko kupigana na kuumizana. 

Tukio hili limetokea siku mbili tu baada ya mtandao huu wa Malunde1 blog kuripoti kuhusu Mwanamke kumuua kwa kumchinja mme wake huko katika kata ya Tinde wilayani Shinyanga,kutokana na ugomvi wa simu ya mkononi,mke akimtuhumu mme kupigiwa na mchepuko wake.

Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Rukwa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com