Mbunge wa Jimbo la Geita Joseph Kasheku Msukuma akiwa na wenzake wakielekea mahakamani.Picha zote na Joel Maduka
Mbunge Msukuma akisalimiana na wananchi wakati akiingia ndani ya mahakama.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita,Bi Khadja Said na Diwani wa viti maalum Bi,Mahimuna Mingisi wakiingia ndani ya mahakama.
Mbunge Msukuma akitoka Nje ya mahakama baada ya kupatiwa dhamana.
Mbunge wa Jimbo la Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Geita Joseph Kasheku Msukuma akiwapungia Mkono wananchi waliokuwa nje ya mahakama baada ya kutoka ndani ya mahakama ya hakimu Mkazi Mkoani Geita kwa dhamana ya Sh,Milioni Tano pamoja na viongozi wengine.
Wananchi wakiwa nje ya mahakama
****
Mbunge wa Jimbo la Geita Joseph Msukuma na madiwani 7 wa halmashauri ya Mji wa Geita na Wilaya ya Geita pamoja na mwananchi mmoja jana Jumanne Septemba 19,2017 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita na kusomewa mashtaka manne yanayowakabili.
Kwa nyakati tofauti kuanzia Septemba 14 hadi 17 walikamatwa na polisi wakituhumiwa kuhusika kufunga barabara za kuingia kwenye mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM).
Septemba 14 madiwani wa halmashauri mbili za Wilaya ya Geita walifunga barabara zinazoingia GGM wakishinikiza kulipwa Dola 12 milioni za Marekani zinazotokana na ushuru wa huduma.
Mbali na mbunge huyo,washitakiwa wengine waliofikishwa mahakamni hapo ni Madiwani Costantine Morandi, Winfrida Malunde, Ngudungu Joseph, Martin Kwilasa, Hadija Said, Michael Kapaya, Maimuna Mengisi na Steven Werema ambaye ni mwananchi.
Mbele ya hakimu Mkazi mfawidhi Ushindi Swalo, upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Emily Kiria na Hezron Mwasimba, Wakili Hezron amesema Septemba 14 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi washtakiwa hao wanadaiwa kufanya mkutano usio halali, kula njama, kuziba barabara na kuharibu Bomba la maji kutoka Ziwa Viktoria kwenda kwenye mgodi wa GGM.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washitakiwa wote wamekana kuhusika na vitendo hivyo na wameachiwa kwa dhamana ya Sh Milioni 5 huku kila mshitakiwa akitimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja.
Aidha kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 10 mwaka huu.
Chanzo-Maduka online