Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : MKURUGENZI WA NAMAINGO AGENCY CO. LTD AZINDUA MRADI WA UFUGAJI KUKU WA WAJASIRIAMALI WA SHINYANGA,KISHAPU NA KAHAMA 'SHIKIKA'

Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd imezindua Mradi mkubwa wa ufugaji kuku unaosimamiwa na Kikundi cha Ujasiriamali cha Shinyanga,Kishapu na Kahama (SHIKIKA) uliopo katika mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo Jumatatu Septemba 18,2017 katika mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha manispaa ya Shinyanga.

Kikundi cha SHIKIKA kinachotekeleza mradi huo,kilianzishwa Machi 16,2017 baada ya kampuni ya Namaingo Business Agency Co.Ltd kuwaelekeza wanachama wake kuunda vikundi vya wanachama hamsini hamsini ili wakubaliane kuendesha mradi wanaoupenda.

Wanakikundi hao waliamua kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku wa kienyeji ndipo kampuni hiyo ikawachangia vifaranga 200,wakaanza ufugaji tarehe 9.6.2017 na mpaka sasa kikundi kina kuku zaidi ya 1300.

Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim aliwapongeza wanakikundi hao kwa kuchangishana fedha shilingi milioni 8 na kuamua kuanzisha mradi huo.

“Ndugu zangu jambo hili mlilofanya na mlilolitekeleza kwanza ni jambo la kitaifa kwa sababu wananchi wakiwa na uchumi mzuri serikali nayo inapata kodi lakini pia tunakuwa tumetengeneza ajira”,alisema Ibrahim.

“Pamoja na jitihada hizi mlizochukua kwa muda mfupi,Tunatamani kuona kila mtu anakuwa na kuku walau 1000 kwenye banda lake,najua changamoto kubwa iliyopo ni mitaji na riba kubwa kwenye mikopo lakini kuna fedha kwa ajili ya maendeleo ya akina mama na vijana zenye riba ndogo sana zipo kwenye benki mbalimbali,serikali inafanyia kazi suala la mikopo hiyo”,aliongeza.

Aidha Ibrahim aliwataka wananchi kuwa na maamuzi ya kutoka katika hali walizonazo kwa kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa na kuilaumu serikali.

“Hakuna haja ya kuilaumu serikali bali unapaswa kujiajiri ili kubadilisha maisha yako,hakuna maisha mazuri kama mtu ukijiajiri,hata hao waliojiriwa wakistaafu huwa wanarudi kujiajiri hivyo kujiajiri ndiyo kila kitu katika maisha yako”,aliongeza Ibrahim.

“Sisi Namaingo Bussiness Agency Co. Ltd kazi yetu ni kuwabadilisha kiakili ili muweze kubadilika kimawazo kwani fursa za kubadili maisha yenu,zipo nyingi,kufanikiwa kwa mtu ni maamuzi ya mtu mwenyewe”,alisema.

Akisoma risala, Katibu Msaidizi wa SHIKIKA,Beatrice Nangale alisema gharama za kuanzisha mradi huo ni shilingi milioni 8 lakini mpaka sasa umegharimu shilingi milioni 20 ambazo ni michango ya wanachama.

Alisema ili kufikia malengo yao,kundi hilo linahitaji eneo kubwa la ekari 3000 kwa ajili kupanua mradi wa kuku,kuwa na mashine za kutotolea,kutengeneza chakula cha kuku,kuchakata minofu ya kukuna ufugaji wa nyuki wa asali.

“Pia tunataka kufuga samaki,mbuzi,sungura na ng’ombe kisha kusindika nyama zao,kulima mboga mboga na matunda kama vile mapapai,kupanda miti na kujenga nyumba kwa ajili ya makazi”,alifafanua Nangale.

Hata hivyo alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa chakula na dawa za kuku mjini Shinyanga,masharti magumu ya benki za utoaji mikopo,ukosefu wa wataalam wa masuala ya mifugo pamoja na kukosa wahisani na misaada ya wahisani kutokana na hali ngumu za kiuchumi za wanakikundi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamaguha Deo Masalu alisema mradi huo utatumika kama shamba darasa na kuahidi serikali kuwapa ushirikiano wanachama wa kikundi ili kuhakikisha wanafikia malengo yao.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akijiandaa kukata utepe kwa ajili ya kuzindua mradi wa kuku unaosimamiwa na Kikundi cha Ujasiriamali kutoka Shinyanga,Kishapu na Kahama (SHIKIKA) leo Septemba 18,2017.Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog 
Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akikata utepe.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akishikana mkono na Katibu wa SHIKIKA,Gelard Egwaga baada ya kukata utepe.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akiangalia kuku wenye umri wa miezi miwili katika moja ya mabanda ya kundi la SHIKIKA.
Viongozi wa kundi la SHIKIKA wakimwongoza Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim kuangalia kuku hao.
Ndani ya banda la kuku,mgeni rasmi Biubwa Ibrahi na waangalizi wa kuku (vijana watatu kulia).
Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akiwa amebeba jogoo mwenye umri wa miezi minne katika banda la kuku.
Kuku wakiwa katika banda.
Katibu wa SHIKIKA,Gelard Egwaga akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wao wa ufugaji kuku unaosimamiwa na SHIKIKA.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuku unaosimamiwa na SHIKIKA.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akisisitiza umuhimu wa kujiari badala ya kutegemea kuajiriwa na serikali.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akizungumza. 
Mwenyekiti wa SHIKIKA,Kiyungi Mohamed Kiyungi akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Wanachama wa SHIKIKA wakiwa eneo la tukio.
Wanachama wa SHIKIKA wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea.
Uzinduzi wa mradi unaendelea. 
Mratibu wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd mkoa wa Shinyanga,Vaileth Kyando akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa ufugaji kuku.
Katibu Msaidizi wa SHIKIKA,Beatrice Nangale akisoma risala kwa niaba ya wanachama wa SHIKIKA.
Wa kwanza kushoto ni Afisa Mtendaji wa kata ya Chamaguha,Deo Masalu,Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim na Katibu wa SHIKIKA,Gelard Egwaga wakifuatilia kwa umakini risala kutoka kwa Katibu Msaidizi wa SHIKIKA,Beatrice Nangale.
Makamu mwenyekiti wa SHIKIKA,Aneth Muro akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa ufugaji wa kuku.
Afisa Mtendaji wa kata ya Chamaguha,Deo Masalu akizungumza wakati uzinduzi wa mradi wa ufugaji kuku unaotekelezwa katika kata yake.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com