SEKONDARI TATU ZA MWANZA ZAPOKEA MSAADA KUTOKA MRADI WA TIGO E-SCHOOLS


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella,akitata utepe wakati wa uzinduzi wa programu ya kompyuta yenye vitabu vya masomo ya shule za sekondari(Tigo eSchool) iliyounganishwa kwenye shule ya sekondari Pamba mkoani Mwanza jana na Kampuni ya Tigo, Kulia ni Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Ziwa Ali Maswanya.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella,akimshukuru Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Ziwa Ali Maswanya(kushoto) baada ya kuzindua programu ya kompyuta yenye vitabu vya masomo ya shule za sekondari(Tigo eSchool) iliyounganishwa kwenye shule ya sekondari Pamba na Kampuni ya Tigo, Jumla ya shule tano za mkoa huo zimeunganishwa na huduma hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella akijaribu huduma ya Tigo eSchool kwenye shule ya Sekondari Pamba mkoani Mwanza. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi wa Tigo kanda ya Ziwa, Alli Maswanya (kushoto)na Mbunifu waTovuti toka Shule Direct, Rajabu Mgeni. 
***
Mwanza 21 Septemba, 2017- Kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali nchini, Tigo Tanzania kupitia mradi wa Tigo E-schools imetoa msaada wa mfumo wa teknologia kwa masomo kumi na moja (11) ya shule kwa sekondari tatu (3) za Mkoani Mwanza.

Ikiwa ni sehemu ya shughuli za jamii zinazoendana na msimu wa Tigo Fiesta 2017 – Tumekusomaa, msaada huu unaonesha sifa kuu ya Tigo kama mtandao unaoelewa wateja wake na kuwapa huduma zinazoendana na mahitaji yao. Kupitia mradi wa Tigo e-schools, Tigo imeona na kuelewa hitaji la wanafunzi la maarifa ya Tehama, na inakutana na hitaji hili kupitia utoaji wa kompyuta zilizounganishwa na intaneti na mifumo mbali mbali ya elimu. 

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi mfumo huo, Meneja Kanda wa Tigo, Ali Maswanya alisema kuwa mfumo huo utawaandaa wanafunzi kuibua fursa na kuwa sehemu ya mabadiliko ya Tehama ulimwenguni. 

‘Dunia ya sasa inaendeshwa kidigitali. Mradi wa Tigo E-shools unawaandaa wanafunzi kuwa sehemu ya ulimwengu huu wa kidigitali. Kupitia mfumo huu, wanafunzi wataongeza busara, kupanua mitazamo na ubunifu wao, na hivyo kuibua fursa pamoja na kukabiliana na changamoto zinazoendana na ulimwengu wa sasa wa digitali,” Maswanya alisema. 

Alitaja shule za sekondari zilizofaidi kutoka kwa msaada huo Mkoani Mwanza ni Shule ya Sekondari Pamba, Sekondari ya Mwanza na Sekondari ya Mirongo. Tigo E-schools pia itasambaza mfumo huo wa elimu kwa shule 52 za sekondari katika mikoa 12 kati ya mikoa 15 ambayo msimu wa Tigo Fiesta 2017 Tumekusomaa utazuru mwaka huu. 

Mwaka 2016, Tigo ilifanya makubaliano na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwezesha kusambazwa kwa mtandao katika shule za sekondari nchini ili kuchangia mpango wa miaka miwili wa serikali kuleta mabadiliko ya elimu kwa njia ya mtandao. 

Kama sehemu ya makubaliano hayo, Wizara ilitoa majina ya shule zisizokuwa na maabara ya kompyuta na pia kutoa mwongozo wa utekelazaji wa mradi huo. Tigo ilishiriki katika ujenzi na kuunganisha maabara mpya za kompyuta na mtandao, na hatua ya tatu ni ya kuunganisha shule husika na teknologia hii ya elimu kwa njia ya mtandao. 

“Kupitia mpango wetu endelevu wa kuwekeza katika hudma za jamii, Tigo inachangia jitahada za serikali za kuigeuza Tanzania kuwa na uchumi wa maarifa ifikapo mwaka 2025.” Maswanya aliongeza. 

Shule ambazo zitaunganishwa na mfumo huo wa elimu kwa njia ya Tehama ni Arusha Day, Ilbouru na Arusha Sekondari mkoani Arusha; Mwanza, Pamba na Mirongo Sekondari mkoani Mwanza; Tabora Girls na Milambo Sekondari mkoani Tabora; na Mpwapwa Sekondari mkoani Dodoma. 

Shule nyingine ni Iringa na Kleruu Sekondari mkoani Iringa; Matalawe na Songea Girls Sekondari mkoani Songea; Njombe na Mpechi Sekondari mkoani Njombe; Morogoro Municipal na Mzumbe Sekondari zilizopo Morogoro; pamoja na Handeni na Shemsanga Sekondari huko Tanga. 

Shule nyingine zitakazofaidi mfumo huu wa elimu kutoka Tigo e-schools ni Lyamungo Sekondari na Machame Girls Sekondari huko Moshi; Newala Day na Masasi Day Sekondari zilizopo Mtwara na kwa mkoa wa Dar es Salaam, sekondari za Mbagala, Kibamba, Benjamin Mkapa na Makumbusho zitaunganishwa na mfumo huo wa elimu kwa njia ya Tehama. 

‘Kwa mara nyingine, natoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Tanzania kwa kuiruhusu Tigo Tanzania kuwa sehemu ya mipango yake ya kuiingiza Tanzania katika mfumo wa uchumi wa maarifa,’ Meneja huyo wa Tigo alimaliza.

Tigo ni mdau muhimu wa elimu na imetoa michango mbali mbali kuinua viwango vya elimu nchini. Mwaka jana Tigo ilichangia madawati zaidi ya 7,100 katika shule za mzingi nchini kote. Vilevile Tigo imetoa kompyuta 77 zilizounganishwa na mtandao wa kasi zaidi wa Tigo kwa vituo vya elimu ya juu nchini. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post