WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema serikali ipo tayari kuhudumia kwa kiasi chochote cha fedha matibabu ya kibingwa kwa ajili ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), endapo itapokea ombi rasmi kuanzia sasa.
Amesema kimsingi serikali haijapokea ombi lolote rasmi kutoka kwa familia lililoambatana na taarifa ya madaktari kuthibitisha kiongozi huyo anahitaji huduma za matibabu ya kibingwa zaidi katika nchi yoyote duniani, licha ya kwamba imekuwa tayari kufanya hivyo mara moja tangu lilipotokea tukio la kujeruhiwa kwa risasi mbunge huyo.
Alitoa kauli hiyo alipozungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Tanga uliolenga kutoa ufafanuzi kwa Watanzania pamoja na familia ya Lissu kuhusu msimamo wa serikali katika matibabu ya kiongozi huyo.
Ummy ambaye yuko jijini Tanga kwa shughuli za kikazi za uchaguzi wa jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema wizara yake imeona ni vema kuzungumzia suala hilo kutokana na kuibuka kwa taarifa mbalimbali zinazolenga kupotosha jamii na ulimwengu kuhusu matibabu ya Lissu yanaoendela katika hospital iliyoko Nairobi nchini Kenya.
“Naomba nichukue nafasi hii kuwajulisha Watanzania kwamba serikali haijakataa wala haijashindwa kugharamia matibabu ya Mheshimiwa Lissu kama inavyodaiwa na baadhi ya watu hivi sasa, taarifa tunazopata mpaka sasa kiongozi hiyo anaendelea na matibabu yake huko Nairobi, lakini kidogo tunaona kunafanyika mambo yasiyoeleweka ikiwemo hasa dhamira ya kufanywa kwa mambo hayo, hivyo naomba kupitia mkutano huu mfikishe ujumbe kwamba serikali iko tayari kumhudumia popote duniani anapotaka kupelekwa kupata matibabu ya kibingwa endapo tu tutapata maombi rasmi kutoka kwa familia yake,” alieleza waziri huyo.
Alisema upo utaratibu maalumu ambao serikali inawajibika kuufuata ili kumsaidia Mtanzania yeyote anayehitaji matibabu ya kibingwa nje ya nchi, lakini tofauti iliyojitokeza kwenye suala la Lissu baada ya kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ndugu na jamaa zake ndiyo waliomchukua kumpeleka Kenya.
“Pamoja na nia ya serikali ya kutaka kumpeleka Lissu katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa Muhimbili, ndugu na jamaa wa karibu walifanya majadiliano na kuamua badala ya kupelekwa huko na serikali wao walipenda kumpeleka Nairobi... hivyo kama serikali hatukuwa na uamuzi wowote au nguvu zaidi ya kumzuia mgonjwa huyo asipelekwe katika hospitali ya Nairobi hivyo mgonjwa aliruhusiwa kuondoka usiku huo huo majira ya saa tano na nusu usiku kwa ndege,” alieleza.
Aliongeza kuwa pamoja na mambo yote hayo, si vema suala la matibabu ya Lissu likaendelea kuchukuliwa kisiasa hasa kwa kuendelea kusambaza taarifa za upotoshaji kwa jamii wakati utaratibu wa serikali upo wazi na unafahamika.
Akizungumzia michango mbalimbali ya fedha inayoendelea kuhamasishwa na watu mbalimbali nchini, waziri ameiomba familia hususan mke wa Lissu kuwasiliana moja kwa moja na serikali ili kueleza mahitaji ya mahali popote duniani wanapotaka kumpeleka mgonjwa wao ili kuokoa maisha yake.
“Serikali inahudumia matibabu yake pale inapohitajika kwa sababu licha ya kuwa ni Mtanzania, lakini ieleweke kwamba Lissu ni mbunge, lakini cha kushangaza tumeona inapitishwa michango kadha wa kadha inayolenga kukusanya fedha za matibabu hatuelewi michango hiyo inaweza kutumika vibaya, kiutapeli wakati serikali hatujashindwa kutekeleza jukumu hili,” alifafanua waziri mwenye dhamana ya Afya.
“Nimuombe mke wa Lissu, dada Alice najua uko katika wakati mgumu sana, lakini naamini utaifikia serikali ili kuhakikisha kwamba tunamsaidia Lissu apate matibabu katika nchi yoyote duniani iwe India, Ujerumani au popote duniani serikali itagharamia,” aliongeza.
Spika Job Ndugai alitangaza bungeni kwamba wabunge wote wana bima ya afya na kwamba wanatibiwa katika hosptali ya Taifa ya Muhimbili na kama kuna ulazima wa kupelekwa nje ya nchi, wabunge wote hutubiwa katika hosptali ya Apollo ya India.
Alisema familia ya Lissu ndiyo iliyoomba kumpeleka Nairobi. Naye Mwandishi Wetu, Katuma Masamba anaripoti kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema Mahakama haiwezi kutoa maoni kwa jambo ambalo liko kwenye utaratibu wa kufikishwa mahakamani, kwa kuwa kanuni za mahakama haziruhusu jambo hilo.
Jaji Juma alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali kuhusu ukimya wa mahakama juu ya tukio tukio la Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupigwa risasi na barua ya Chama cha Wanasheria wa Marekani ya kulaani tukio hilo, huku akitaka jamii kutulia na kuachia mamlaka husika kufanya kazi yake.
Akijibu maswali ya wanahabari jana Dar es Salaam, Jaji Juma alisema kanuni za mahakama haziruhusu jambo ambalo litakuja mahakamani kutolewa ushahidi, kuongelewa au kutolewa maoni kwa kuwa ni kinyume cha kanuni.
Kuhusu uhuru wa mahakama, alisema mahakama ziko huru na hakuna jaji yeyote anayeweza kumuingilia hakimu yeyote na kumueleza namna ya kufanya na kwamba mhimili huo unafanya kazi zake kwa uwazi kuliko mihimili mingine. Katika hatua nyingine, Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuia ya Madola (CMJA) utafanyika Dar es Salaam kuanzia Jumatatu.
IMEANDIKWA NA ANNA MAKANGE - HABARILEO TANGA
Social Plugin