Sehemu ya mzigo wa almasi uliokamatwa ambao thamani yake ni zaidi ya Shilingi bilioni 64.
****
ALMASI zenye uzito wa kilogramu 29.5 za thamani ya zaidi ya Sh bilioni 64, ambazo zilibakiza dakika tano tu kutoroshwa kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (JNIA) kwenda ughaibuni, zimetaifi shwa na serikali.
Aidha, watumishi wa serikali na maofisa wa Mgodi wa Almasi wa Williamson wa Mwadui Shinyanga, waliohusika na uthaminishaji wa awali wa almasi hizo na kudanganya kuwa zilikuwa na uzito wa kilogramu 14 tu, watachunguzwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa akipokea ripoti ya timu ya wataalamu, iliyoundwa kuchunguza upya uzito na thamani halisi ya almasi hizo baada ya kuzikamata katika uwanja huo wa JNIA Agosti 31, mwaka huu.
Uthamini uliofanywa awali kwa almasi hiyo, iliyokuwa mbioni kupakiwa ndani ya ndege kutoroshewa nchini Ubelgiji, ulieleza kuwa ilikuwa na thamani ya chini ya Sh bilioni 32, huku ikielezwa pia kuwa na kilogramu 14, taarifa zilizogundulika kuwa zilikuwa ni za uongo.
Jana Waziri Mpango alipokea maelezo ya almasi hiyo kutoka kwa Kiongozi wa Jopo la Wataalamu waliofanya uthamini mpya, Profesa Abdulkarim Mruma na wasaidizi wake. Baada ya kuridhika na maelezo, yaliyodhihirisha kuwepo kwa kiwango cha juu cha udanganyifu kuhusu uzito na gharama za almasi hiyo, kwa lengo la kuliibia taifa, Waziri Mpango aliagiza almasi hiyo yote kutaifishwa, kupigwa mnada na fedha zitakazopatikana kuingia serikalini.
Aliagiza pia kuwajibishwa kwa maofisa wa serikali waliohusika katika udanganyifu huo kwa wahusika hao kukamatwa, kuchunguzwa mali zao ikiwemo majumba, mashamba, magari kuona kama vinaendana na mishahara yao na baadaye kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Alisema, Watanzania wamechoshwa kuona mali zao zikiibiwa kila kukicha huku serikali ikikosa mapato makubwa kutokea katika rasilimali hizo. Pia, aliagiza kuandaliwa kwa wataalamu wa madini na wapelekwe kwenye migodi haraka, kukabiliana na wizi wa aina hiyo, huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na wizi wa aina hiyo.
Waziri Mpango aliagiza pia upimaji wa madini kufanyikia kwenye eneo la migodi, na pia kununuliwa kwa mashine za kupimia madini kwenye maeneo ya migodi, baada ya kuelezwa na Profesa Mruma kuwa ukosefu wa vifaa vya kupimia ni chanzo cha udanganyifu huo.
“Kazi nzuri sana umefanya Professa Mruma na wenzako na kwa sasa ninaagiza haya madini tuliyokamata hapa, kulindwa kuanzia hapa hadi pale yatakapoingizwa sokoni, pia ninamtaka Gavana wa Benki Kuu (Profesa Benno Ndulu) kuanza kuhifadhi madini ya vito na si fedha peke yake.
“Inashangaza kuona maofisa wa juu wa Wizara ya Nishati na Madini waliokuwa na jukumu la kuthaminisha madini haya wamedanganya huku wale walio chini yao wametoa tathmini ya kweli, sasa huu ndiyo uzalendo unaotakiwa,” aliongeza Dk Mpango.
Kwa upande wa Mgodi wa Williamson Diamond LTD, Waziri Mpango alisema kutokana na kubainika kujihusisha na udanganyifu, huku kampuni hiyo ikieleza kupata hasara kila mwaka, kuanzia mwaka huu itawajibika kutoa gawio serikalini na alimuagiza Profesa Mruma kuijulisha Bodi ya Kampuni hiyo agizo hilo la serikali mara moja.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salam, Lazaro Mambosasa akizungumzia agizo hilo, alisema kuwa hakuna mtuhumiwa ambaye hatoshughulikiwa katika kosa hilo.
Alisema sheria itafuata mkondo na kuwa kila mtu ambaye ameshiriki kwa namna moja au nyingine, atakamatwa kuanzia wale waliopo mgodini hadi wale walioshiriki katika kutaka kutorosha madini hayo.
Ulinzi mkali kisanduku cha almasi Katika tukio hilo, lililorushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha TBC 1, kwa lengo la kuwaonesha wananchi namna madini yao yanavyohujumiwa, kilioneshwa kisanduku kidogo kilichohifadhia madini hayo ya mabilioni ya shilingi, kikiwa katika chumba chenye ulinzi mkali.
Kabla ya lango la chumba hicho kufunguliwa, alionekana mlinzi akiwasiliana na watu mbalimbali ili kupata ruhusa ya kufungua lango hilo licha ya kuwa mbele yake alikuwepo Waziri wa Fedha na maofisa wa juu wa serikali na vyombo vya dola, hatua inayodhihirisha kuwepo kwa mfumo thabiti wa kulinda almasi hizo.
Baada ya takribani kama dakika 30 za kuwasiliana na watu wasiojulikana, hatimaye mlinzi huyo alisomewa tarakimu, ambazo alianza kuziingiza katika kufuli la mlango huo na hatimaye ulifunguka na kuwawezesha viongozi hao wa serikali kuingia ndani.
Mlinzi huyo alitajiwa namba kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza alitajiwa namba tisa tofauti na kisha kuja kutajiwa namba tano tofauti na alipoingiza sefu hiyo ilifunguka, na bado mlinzi huyo akafungua tena kufuli kadhaa, kabla ya kutoa kisanduku hicho cha mbao kilichokuwa na madini hayo ya almasi.
Hata baada ya kukifikia, bado haikuwa kazi rahisi kukifungua kisanduku hicho kwani kilikuwa kimefungwa na makufuli mawili yenye lakiri; na iliwachukua Profesa Mruma na wenzake zaidi ya dakika 15 kuvunja makufuli na lakiri hizo na baadaye kufungua skurubu nne kwa kutumia bisibisi, hatimaye kutoa madini hayo.
Ingawa zilikuwa ndani ya vifuko vya plastiki vyeupe, lakini kwa mara ya kwanza Watanzania wengi waliokuwa wakifuatilia matangazo ya televisheni waliweza kujionea utajiri wa rasilimali zao, na katika tukio la kushangaza zipo almasi ambazo zilikuwa zikitoa nuru, iliyokuwa ikinakisi kioo cha miwani ya Waziri Mpango na kutoa mwangaza wa kupendeza.
Baadaye Profesa Mruma na jopo lake, walianza kutoa maelezo ya kitaalamu ya almasi hiyo, wakisema zipo za aina tatu; za daraja la kwanza ambazo ni kubwa zikiwa zimechimbwa moja kwa moja mgodini, za daraja la pili zenye ukubwa wa kati na za daraja la tatu ambazo ni ndogo ndogo kama punje za sukari ambazo zinapatikana kwa njia ya kuchekecha masalia ya almasi (Makinikia).
Walimuonesha Waziri pia kifuko chenye almasi za rangi ya pinki, zinazopatikana Tanzania peke yake kwenye mgodi huo wa Williamson Diamond wa Mwadui, Shinyanga, ambazo ndizo zilizokuwa zinatoa mwangaza uliokuwa unaakisi katika miwani ya waziri na kutoa mwangaza ambao zinaweza kuonekana hata kama kuna giza.
Viongozi wengine walioandamana na Dk Mpango jana ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Charles Kichere, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Biswalo Mganga, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Brigedia Jenerali John Mbungo, Kamishina wa Madini Benjamin Mchwampaka na Kamanda Mambosasa.
Ukaguzi huo ni mwendelezo wa harakati za Rais John Magufuli za kukabiliana na wizi wa rasilimali za nchi, ambapo mapema wiki hii alipokea ripoti kutoka kamati mbili za Bunge, zilizochunguza biashara za madini ya Tanzanite na almasi na kubaini udanganyifu, uzembe, rushwa na ubadhirifu mkubwa.
Ripoti za Kamati hizo zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai zilitanguliwa na ripoti kuhusu Tume mbili zilizoundwa na Rais ili kuchunguza kiwango cha madini ya dhahabu, kinachopatikana kwenye mchanga wa masalia ya dhahabu (Makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi na athari zake kiuchumi, tume zilizobaini Taifa kuhujumiwa kwa kiwango kisichovumilika.
IMEANDIKWA NA EVANCE NG'INGO- habarileo