Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amefunguka na kusema
watu ambao wamefanya uhalifu wa kumpiga risasi Mbunge wa Singida
Mashariki Tundu Lissu wanaweza patikana ikiwa wananchi watasaidia jeshi
hilo kupata taarifa za wahalifu hao.
IGP Sirro amesema hayo leo alipokutana na waandishi wa habari akielezea hali ya usalama wa nchi na kudai usalama wa nchi upo vizuri na kuwa mpaka sasa jeshi la polisi limeongeza nguvu ya upelelezi mjini Dodoma ili kuhakikisha linawapata watu ambao wamefanya uhalifu wa kumpiga risasi mbunge Tundu Lissu , huku akiwataka wananchi wasihusishe tukio hilo na masuala ya kisiasa.
"Naomba wananchi wasidanganywe kwenye suala zima la siasa na vitu vingine hapa huwa nasema siku zote kama hakuna amani na usalama siasa haiwezi kupata nafasi
"Hili tukio limetokea tunapeleleza na tupo makini na hili tukio, kwa sasa tumeongeza vikosi vya upelelezi Dodoma, wale waliofanya lile tukio ni lazima tutawakamata ila upelelezi huu unaweza kuzaa matunda mazuri zaidi endapo wananchi watatupa ushirikiano wa kutosha" alisema IGP Sirro
Aidha IGP Sirro amezungumzia kuhusu moja ya kauli ya Tundu Lissu ambayo aliwahi kusema kuwa kuna watu wanamfuatilia na kuvitaka vyombo vya usalama kuacha kuwatuma watu hao kumfuatilia na kudai kuwa hakuwahi kuripoti katika kituo chochote cha polisi, na kusema sasa usiwe wakati wa kuzungumzia jambo hilo.
IGP Sirro alimalizia kwa kusema kuwa jeshi la polisi lipo imara na lipo kwa ajili ya kulinda watanzania pamoja na mali zao na si kuwamumiza watanzania hivyo ametoa rai kwa wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kuwapata watuhumiwa hao.
Social Plugin