Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa mshtuko taarifa ya kupigwa risasi mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.
Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki, amepigwa risasi baada ya kikao cha Bunge mchana wa leo Alhamisi.
Shambulio hilo limetokea leo mchana nyumbani kwa Lissu, Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
“Chadema tunalaani vikali kitendo hicho na tunafuatilia kwa karibu hali yake,” imesema taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Uenezi, Mawasiliano na Mahusiano ya Nje ya Chadema makao makuu.
Wakati huohuo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesema umepokea kwa mshtuko taarifa za kupigwa risasi Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).
Mratibu wa mtandao huo, Onesmo ole Ngurumwa katika taarifa amesema wanatoa pole kwa familia ya Lissu, wananchi wa Singida Mashariki, wanachama wa TLS na Watanzania kwa jumla.
Mtandao huo umewahimiza Watanzania wote kumwombea Lissu.
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako Lissu anaendelea na matibabu.
Pia, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amefika hospitalini hapo ambako Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, James Charles amesema Lissu yu hai na imara.
Dk Charles akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita amesema mbunge huyo amepigwa risasi tumboni na kwamba timu ya madaktari inaendelea na matibabu.
Social Plugin