Na.Paschal Dotto-MAELEZO.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhiwa mashine maalumu ya kutoa dawa za usingizi kwa mama wajawazito wenye uzazi pingamizi wakati wa upasuaji kwaajili ya kuokoa maisha yao.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Jijini Dar es Salaam Waziri mwenye dhamana ya Afya Mh.Ummy Mwalimu alisema kuwa, hiyo ni hatua kubwa katika kupambana na vifo vya wakina mama wajawazito pamoja na watoto wachanga.
Waziri Ummy alitoa pongezi kwa watu waliojitolea kupanda mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuunga mkono kampeni ya kuokoa maisha ya mama na mtoto wakiongozwa na Dkt.Ahmed Mohamed Makuwani, ambapo alisema kuwa waliopanda mlima Kilimanjaro wamewezesha kupatikana kwa msaada wa mashine hiyo, hivyo akawashukuru na kuomba wadau wengine kuiga mfano huo.
“Tunawashukuru Utepe Mweupe wa Uzazi Salama kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya katika kushirikiana na serikali ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo kwa watoto wachanga, hatua hii inatufariji sana na naomba watanzania na wasio watanzania wenye mapenzi mema na afya ya mama na mtoto kuendelea kusaidia juhudi hizi ”, alisema Waziri Ummy.
Akieleza mafanikio katika sekta ya Afya waziri Ummy alisema kuwa kuna zaidi ya vituo vya afya 480 nchi nzima na kati ya hivyo vituo 109 vinavyumba vya upasuaji ambayo ni sawa na asilimia 20 huku akibainisha kuwa kufikia Juni, 2018 serikali inatarajia kujenga vyumba vya upasuaji 170 vitakavyosaidia upasuaji wa mama wenye uzazi pingamizi na idadi hiyo itaongezeka na kufikia vituo 279.
Aidha Waziri Ummy alisema kuwa licha ya kujenga vyumba hivyo watahakikisha upatikanaji wa vifaa, ujenzi wa maabara kubwa, wodi za kinamama pamoja na nyumba moja ya mtumishi katika vituo vya afya vyenye vyumba vya upasuaji.
Kutokana na mpango mkakati wa kupambana na vifo vya wajawazito na watoto wachanga Serikali inatarajia kufikia asilimia 50 mpaka asilimia 80 ifikapo mwaka 2020 ambayo ni kampeni ya Serikali ya Awamu ya Tano inayotarajia kuzinduliwa hivi karibuni ijulikanayo kama ‘Jiongeze Tukuvushe salama’ kampeni ambayo inalenga kuwasaidia wakina mama wajawazito popote walipo ili kuokoa maisha yao.
Naye Mratibu wa Utepe Mweupe Dkt. Rose Mlay alisema kuwa mashine hiyo ni maalum katika kunusuru maisha ya mama na mtoto lakini pia inaweza kutumika kwa mtu yeyote mwenye matatizo ya kufanyiwa upasuaji.
Kwa upande wake katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya alisema mashine hiyo iliyotolewa na shirika la the Guardian Health yenye themani ya Shilingi milioni 55 ina ubora na kiwango cha kutosha katika kutoa huduma kwa mgonjwa wakati wa upasuaji.
“Mashine hii ni ya kipekee kwa sababu ina uwezo wa kutengeneza oksijeni na haihitaji mitungi ya gesi kwa hiyo ni mashine nzuri kwa wagonjwa na akinamama wenye uzazi pingamizi”, alisema Dkt.Mpoki.
Dkt. Mpoki alisema kilichopo sasa ni kufundisha wataalam watakaohusika na matumizi ya mashine hiyo ili waweze kuitumia ipasavyo na kuahidi kuwa atahakikisha inatunzwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.