Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimesema kimepokea kwa mshtuko na masikitiko tukio la Rais wa chama hicho, Tundu Lissu la kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake Dodoma jana Alhamisi mchana.
Katika taarifa kwa umma, TLS imesema inamuombea kwa Mungu azidi kumlinda na kumhifadhi Lissu ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.
“Kwa vyovyote vile, hivi sasa bado ni mapema sana kujua ni nani hasa wahusika wa tukio hili la kinyama na dhamiri yao, lakini, kwa niaba yetu na wanachama wetu, mawakili wa Tanganyika, tunalaani na kukemea vikali kitendo hiki cha kihalifu,” imesema taarifa ya Godwin Ngwilimi, Makamu wa Rais wa TLS kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa chama hicho.
TLS imetoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi kwa umakini, haki na weledi ili kuwapata watu waliohusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Sisi kwa upande wetu tunalifuatilia suala hili kwa ukaribu na tutaendelea kuufahamisha umma kinachoendelea,” imesema TLS.
Wanasheria hao wametoa pole kwa familia ya Lissu, ndugu na jamaa zake, wanachama wa TLS na Watanzania wote ambao wameguswa na tukio hilo.
“Tunaomba kila mmoja wetu kwa imani yake amuombee ndugu yetu Lissu apone na apate nafuu haraka ili tuungane naye tena katika shughuli zetu za kila siku,” imesema TLS.
Wanasheria hao wamewaomba wanachama na Watanzania wote waendelee kuwa wavumilivu na watulivu.
Social Plugin