Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA WAWILI WATUPWA JELA MAISHA KWA KUMBAKA MKE WA MTU KWA ZAMU

Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imewahukumu kifungo cha maisha jela washtakiwa wawili baada ya kupatikana na hatia katika makosa matatu ya kubaka kwa zamu, kulawiti na kujeruhi.

Washtakiwa Fabian Charles (18) maarufu Kisigara na Asinani Kondo (22) wakazi wa Pugu kwa Mustafa wanadaiwa kumbaka, kumlawiti na kumjeruhi kwa kumchoma na bomba la pikipiki mwanamke mwenye miaka 26 mbele ya mume wake walipokuwa wakitoka matembezi.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 22 mwaka 2015 katika eneo la Pugu wilayani Ilala.

Hukumu hiyo imetolewa jana Ijumaa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan aliyesema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi wanne waliothibitisha mashtaka pasipo kuacha shaka.

Hakimu amesema katika kosa la kwanza ambalo ni kubaka kwa zamu washtakiwa watatumikia kifungo cha maisha jela.

Kwa shtaka la pili la kulawiti washtakiwa kwa pamoja wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Kisigara ambaye katika shtaka la tatu anashtakiwa kwa kujeruhi amehukumiwa kutumikia kifingo cha miaka mitano jela.

Akichambua baadhi ya ushahidi uliotolewa mahakamani, Hakimu Hassan amesema washtakiwa wakiwa na wenzake ambao hawajafikishwa mahakamani walimbaka mlalamikaji kwa zamu usiku akitoka matembezini na mume wake.

Amesema washtakiwa walimvuta mwanamke huyo na kumpelekeka kwenye nyumba ambayo ujenzi wake haujaisha ambako walimbaka kwa zamu na kumlawiti, huku wakichana nguo alizokuwa amevaa.

Hakimu amesema baada ya vitendo hivyo, Kisigara alimjeruhi kwa kumgandamiza kwenye pikipiki na kusababisha aunguzwe na bomba mguu wa kushoto na kupata majeraha.

Awali, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria kwa kuwa kitendo walichomfanyia ni kibaya na ni cha kikatili.

Kabla ya kutolewa adhabu, Mahakama ilitoa nafasi kwa washtakiwa kujitetea, ambao kwa nyakati tofauti waliomba adhabu ipunguzwe kwa kuwa wana familia zinazowategemea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com