Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFUASI WA CHADEMA KANDA YA SERENGETI WATOA TAMKO KUMLAANI MTU ASIYEJULIKANA



Katibu wa CHADEMA kanda ya Serengeti, Renatus Nzemo akitoa tamko rasmi mbele ya waandishi wa habari (hawako pichani) la kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa risasi kwa Tundu Lissu. Kulia kwake ni diwani wa kata ya Ndala, manispaa ya Shinyanga, William Shayo na kushoto kwake ni Emmanuel Ntobi, diwani kata ya Ngokolo.
Wanachama na viongozi wa CHADEMA wakiwa nje ya Ofisi ya Kanda ya Serengeti mjini Shinyanga wakiimba wimbo maalumu kulaani tukio la kushambuliwa kwa Tundu Lissu.


WANACHAMA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara wametoa tamko kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa kupigwa risasi mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Katika tamko lao rasmi lililosomwa mbele ya waandishi wa habari mjini Shinyanga wanachama hao wamesema kitendo kilichofanyika kina ishara ya kutaka kuleta machafuko na kuchafua hali ya amani na utulivu iliyodumu kwa miaka kadhaa hapa nchini.

Walisema kitendo cha mtu asiyejulikana kumshambulia mmoja wa viongozi wao mwandamizi ngazi ya kitaifa na akiwa pia rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) kimewashitua wanachama wote wa CHADEMA na kinastahili kulaaniwa na wapenda amani kote ulimwenguni.

Waliendelea kueleza kuwa mataifa yote yaliyoingia machafukoni chanzo chake huwa ni kutokea kwa mtu au watu wasiojulikana ambao huanza kuwaua watu mashuhuri katika taifa husika, na kwamba mtu asiyejulikana ni nabii wa ghasia na mauaji makubwa kwa taifa.

“Kwa mara ya kwanza katika taifa letu, awamu hii ya tano maarufu kama awamu ya Magufuli, tofauti na awamu zingine zote tumepata mtu asiyejulikana anayeteka na kuua viongozi wakisiasa na watu mashuhuri katika nyanja mbalimbali,”

“Historia ya mtu asiyejulikana katika mataifa na jamii mbalimbali ni mbaya sana. Nchini Rwanda, kabla ya mauaji ya halaiki yaliyopoteza uhai wa watu zaidi ya laki nane, alikuwepo mtu asiyejulikana aliua viongozi mbalimbali akiwemo waziri mkuu wa nchi hiyo, Bi. Agathe Uwilingiyimana mnamo Aprili 7, 1994 kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe,”

“Mtu asiyejulikana hakuishia kuua viongozi na watu mashuhuri tu alienda mbali na kulipua ndege ya aliyekuwa rais wa Rwanda wakati huo Bw. Juvenal Habyalimana akiwa pamoja na Rais wa Burundi Cyprian Ntaryamira Aprili 6, 1994, na baada ya mauaji hayo hatimaye yakaripuka mauaji ya kimbari katika hiyo ya Rwanda,” ilieleza sehemu ya tamko.

Kutokana na shambulio hilo wanachama hao wametoa matamka kadhaa wakilitaka Jeshi la Polisi nchini kuyatekeleza na kuliomba liache kuhadaa watanzania kuwa Tundu Lissu kapigwa risasi na mtu asiyejulikana wakati mitandaoni kuna hadi picha za gari lililotumika kumshambulia.

“Tunaomba waelewe sisi wana CHADEMA hatuwaamini na zaidi tunaona wakifanyacho ni maigizo tu, tunaamini wanajua mwanzo hadi mwisho ya kinachoendelea,”

“Tunalikumbusha jeshi la polisi na vyombo vyake vya usalama ya kwamba sisi bado tunapenda amani ijapokuwa inaonekana wao wameichoka amani. Na kama silaha zao zinasiku nyingi hazifanyi kazi, tunawaomba waende Somalia wakapambane na Al-Shabab au Syria wakapambane na Islamic State.”

Pia wanachama hao wameelezea kushangazwa kwao na kitendo cha kushindwa kuwakamata maadui wa watu na wasiopendezwa na harakati za Tundu Lissu (Mb) wakati yeye mwenyewe kila mara amekuwa akikamatwa na kushitakiwa kwa kile kinachodaiwa kufanya makosa kadhaa wa kadhaa.

Tamko hilo limewaomba viongozi wa kidini, wanasiasa wakosoaji wa serikali na watu mashuhuri wa kada mbalimbali ikiwemo sanaa wasiogope kutoa maoni yao juu ya taifa lao hata kama watahisi maoni yao hayatawapendeza watu wasiojulikana.

“Historia inaonesha watu wanaojifanya hawana upande wowote wa kisiasa ndiyo huwa waathirika wa mwanzo ghasia zikiibuka katika Taifa. Tusipowapinga na kupambana na watu wasiojulikana mara zote taifa huingia machafukoni. Na wakati wa machafuko waathirika huwa wengi zaidi ya hawa watakaodhuriwa na watu wasiojulikana. Hivyo tusiogope, tupambane na mtu asiyejulikana hadi tumshinde,” tamko liliendelea kueleza.

Chama hicho kimewaomba makamanda wote wa CHADEMA popote walipo hivi sasa wajipange kisaikolojia, kiafya na kifizikia katika kuisimamia falsafa ya NGUVU YA UMMA.

“Niwakumbushe tu hawajawahi kutokea watu mtu asiyejulikana akashinda falsafa yetu ya Nguvu ya umma. Tunaamini hakuna kitakacho tusaidia na kutuokoa dhidi ya kuuawa, kuteswa na uonevu mbalimbali zaidi ya falsafa yetu,”

“Tujikumbushe popote tulipo kuwa si mwenyekiti Mhe. Freeman Mbowe, si katibu mkuu, Mhe. Vincet Mashinji atatuokoa bali mkombozi wetu ni falsafa yetu, Nguvu ya umma, ni wakati wa kujihoji je, uko tayari kwa nguvu ya Umma? Na kama ukiona hautoshi, nyamaza milele, ukiona unatosha jiandae kisaikolojia hadi kifizikia,” alieleza katibu CHADEMA kanda ya Serengeti, Renatus Nzemo.

Akizungumza katika mkutano huo wa ndani wa utoaji tamko rasmi la kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa risasi kwa Tundu Lissu, Mwenyekiti wa kamati ya madiwani wa CHADEMA katika kanda ya Serengeti na diwani wa kata ya Manispaa ya Shinyanga, Emmanuel Ntobi ameiomba serikali iwapo jeshi la polisi litashindwa, basi iombe msaada kutoka mashirika ya upelelezi duniani wakiwemo FBI na Scotland yard.

“Tunaiomba serikali iwapo itaona wazi Jeshi lake la polisi hapa nchini litashindwa kuwatambua na kuwakamata watu wasiojulikana, basi wayaombe mashirika makubwa ya kiupelelezi duniani, FBI kutoka Marekani au Scotland yard la nchini Uingereza waje nchini wamsake huyu mtu au watu wasiojulikana,” alieleza Ntobi.

Katika hatua nyingine wanachama hao waliendesha ibada ya maombi kwa ajili ya kumuombea kiongozi wao na mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu ibada zilizoongozwa na Abel Kitalama kutoka dhehebu la KKKT – Shinyanga, na Hamis Ngunila aliyewakilisha waumini wa kiislamu.

PICHA ZAIDI ZA WANACHAMA WA CHADEMA WAKATI WA KUTOA TAMKO LA KULAANI KIONGOZI WAO KUSHAMBULIWA KWA RISASI NA MTU ASIYEJULIKANA.

Dua ya pamoja kabla ya utoaji wa tamko.
Viongozi wakiwa makini wakimsikiliza katibu wa kanda CHADEMA, Renatus Nzemo (wa tatu kutoka kulia).
Diwani wa kata ya Kitangiri manispaa ya Shinyanga, Hamisi Ngunila akiomba dua kwa niaba ya madhehebu ya kiislamu kumuombea Tundu Lissu aweze kupona mapema.


Mmoja wa wanachama ambaye ni muumini wa madhehebu ya kikristo kutoka kanisa la KKKT, Abel Kitalama akiwaongoza wanachama wenzake katika maombi ya kumuombea Tundu Lissu.





Wanachama na viongozi wakiwa katika maombi.


Chanzo-Mtetezi wa Haki Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com