Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI 16,000 HATARINI KUKOSA MIKOPO ELIMU YA JUU 2017/2018


WAKATI mwezi mmoja umebaki kabla ya mwaka mpya wa masomo kuanza kwa vyuo vikuu nchini.


Wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 16,000 kati ya 61,000 walioomba kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wako hatarini kuikosa hata kabla ya zoezi hilo kuanza kutokana na taarifa za maombi yao kuwa na dosari.


Hata hivyo, uongozi wa juu wa bodi hiyo umesema wanafunzi hao bado wana nafasi ya kurekebisha taarifa zao licha ya dirisha la kutuma maombi kufungwa Jumatatu iliyopita.


Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul–Razaq Badru, akizungumza na Nipashe kwa simu jana, alisema hadi siku ya mwisho ya maombi Septemba 11, wanafunzi wanaokadiriwa kuwa 61,000 walikuwa wametuma maombi ya kupewa mkopo kutoka bodi hiyo kwa mwaka ujao wa masomo 2017/18 utakaoanza Novemba.


Alisema kati yao, wanafunzi 16,000 walikuwa na dosari ndogondogo zilizoonekana katika maombi yao, huku wanafunzi wapatao 45,000 wakiwa wamekamilisha vizuri taarifa za maombi hayo.


"Wanafunzi hao bado wanaruhusiwa kurekebisha taarifa zao kwa sababu maombi hufanyika katika mtandao. Bodi bado inafanya uchambuzi wa taarifa," alisema Badru.


Mkurugenzi huyo alizitaja dosari ambazo zimeonekana kwa wanafunzi wengi waliotuma maombi ya mkopo kuwa ni pamoja na kutokuambatanisha vyeti, kuambatanisha cheti ambacho hakijahakikiwa, baadhi ya barua za vyeti vya kifo kutohakikiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).


Alisema bodi hiyo bado inaendelea na uchambuzi wa taarifa za wanafunzi hadi Oktoba 2 utakapokamilika na majina ya waliopangiwa vyuo yatakuwa yameshatolewa.


Badru alisema wanafunzi ambao fomu zao zimebainika kuwa na matatizo, hutumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) na kutakiwa kurekebisha.


Aliongeza kuwa Oktoba 10 majina ya wanafunzi waliopangiwa mikopo yatakuwa yameshafahamika.


Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Tahliso), kupitia kwa Mwenyekiti wake, Stanslaus Kadugalize, ilitoa ombi jana kwa HESLB kutoa nafasi kwa wale wote waliokosea kujaza fomu hizo, ili wafanye marekebisho yanayotakiwa.


"Inawezekana waliojaza vibaya fomu hizo wanatoka katika mazingira magumu ya maisha kiasi cha kushindwa hata kumudu matumizi ya kimtandao," alisema.


"Ili kuepuka kuwaacha walengwa, Tahliso tunaiomba Heslb iliangalie suala hilo kwa jicho la pili, ili kuwapa nafasi kwa mara nyingine."


Alisema kuna uwezekano mkubwa wanafunzi waliokosea kujaza fomu hizo ndio wenye uhitaji mkubwa kuliko waliopatia ujazaji wa fomu hizo.


WENGI WATAKOSA
Mei 13, akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe, aliliambia Bunge wamebaini wanafunzi wengi watakosa mkopo wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2017/18 licha ya kuwa na ufaulu mzuri.


Alisema mwaka jana (2016/17), wanafunzi 48,502 walijaza fomu kwa ukamilifu, lakini 25,555 tu ndiyo walipata mikopo na hivyo kuacha wengine 22,947 wakiwa hawana mikopo kutokana na bajeti iliyotengwa ya Sh. bilioni 427.5 kutotosheleza mahitaji.


Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), alisema mwaka 2017/18, HESLB imeombewa bajeti ya Sh. bilioni 427.5 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi (sawa na bajeti ya mwaka 2016/17) ilhali ufaulu wa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 88 mwaka 2012 hadi asilimia 99 mwaka huu.


"Kamati inaona kwamba, suala la elimu ya juu ni haki ya msingi kwa watu wenye sifa," Bashe alisema, "katika mwaka ujao wa fedha, wanafunzi wengi zaidi watakosa mikopo licha ya ufaulu wao mzuri.


"Kamati inashauri serikali kuongeza bajeti ya HESLB, ili wanafunzi wengi zaidi wanaostahili waweze kupata mikopo kwa maendeleo ya taifa letu."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com