WAZAZI na walezi wenye watoto wenye ualbino katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wamebuni mbinu mpya ya kuwapaka rangi nyeusi watoto wao kwenye ngozi na nywele ili kuwalinda kutofanyiwa vitendo vya ukatili na hata tishio la kuuawa.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Dutwa wilayani Bariadi, George Epafra wakati akielezea mbinu zinazotumika kuwakinga watoto wenye ualbino wakati wa kutambulisha Mradi wa Kukomesha Mauaji na Albino unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Mass Media katika wilaya hiyo.
Epafra alisema kwa sasa baadhi ya vituo vya kulelea watoto wenye ualbino vimefungwa na serikali na watoto hao kukabidhiwa kwa wazazi wao kwa ajili ya kuendelea kuwalea, hivyo jukumu la kuwalinda ili wasifanyiwe vitendo vya ukatili limeachwa juu ya wazazi hao.
“Hivyo watoto wengi sasa wamerudishwa majumbani na idadi kubwa wako maeneo ya kijijini, hivyo ili wazazi na walezi wao waweze kuwalinda ili wasije kufanyiwa ukatili pamoja na kuuawa inabidi wawapake masizi meusi katika sehemu mbalimbali za miili yao huku nywele zikipakwa dawa aina ya piko zionekane ni nyeusi,” alieleza.
IMEANDIKWA NA SHUSHU JOEL, BARIADI
Social Plugin