Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZALENDO YAPIGA JEKI UJENZI WA BWENI SHULE YA NAPS KAGERA


Mwalimu wa taaluma wa shule ya Ngara Anglican Primary School (NAPS) God Marco Gwabunga God Gwabunga (kushoto) akipokea saruji kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Wazalendo Media Productions Limited,Hilali Ruhundwa. 
Mifuko ya saruji iliyotolewa na Kampuni ya Wazalendo Media Productions Limited
Bweni la shule hiyo


Kampuni ya Wazalendo Media Productions Limited ya Dar es Salaam imechangia mifuko saba ya saruji kwa shule ya Ngara Anglican Primary School (NAPS) iliyopo wilayani Ngara mkoani Kagera kwa ajili ya ujenzi wa jengo la bweni shuleni hapo.

Akikabidhi mchango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Bwana Hilali Alexander Ruhundwa amesema kuwa wanatambua umuhimu wa elimu hivyo kama kampuni inayotengeneza faida ni wajibu wao kuchangia maendeleo ya jamii.

"Kampuni yetu imevutiwa na kiwango cha elimu cha NAPS hivyo tumeona tukiwachangia ujenzi wa bweni itasaidia wanafunzi kupata malazi na kupata muda wa kutosha kujisomea",amesema Ruhundwa.

Ameongeza kuwa licha ya shule hiyo kuwa pembezoni mwa nchi lakini inafanya vizuri kitaaluma kuliko hata shule zilizopo jijini Dar es Salaam.

"Makao makuu ya kampuni yetu yapo jijini Dar es Salaam na tungeweza kusaidia kule lakini wao wana uwanda mpana wa kupata wadau wa maendeleo ikilinganishwa na huku Ngara ambapo ni pembezoni mwa nchi",ameongeza.

Akipokea mchango huo, mwalimu wa taaluma wa shule hiyo Bwana God Marco Gwabunga , licha ya kuishukuru kampuni ya Wazalendo kwa mchango huo, amewaomba wadau wengine wa maendeleo hasa wazawa wa wilaya ya Ngara wanaoishi nje ya wilaya hiyo kuwa na moyo wa kuchangia maendeleo nyumbani kwao.

Gwabunga amesema licha ya shule yake kufanya vizuri kitaaluma na kuongoza mkoa wa Kagera kwa shule za msingi, bado wanakabiliwa na changamoto ya kukamilisha ujenzi wa majengo ya bweni.

"Wazazi wengi toka sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi wanatamani kuleta watoto wao kusoma hapa lakini inawawea vigumu kutokana na kukosa sehemu ya malazi",Amesema mwalimu Gwabunga.

Mwalimu Gwabunga ameongeza kuwa wana uhaba wa vifaa hasa mifuko ya saruji 150, vitanda 80, magodoro 160, vifaa vya kuvuna na kuhifadhia maji kwa kuanzia ili wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali wapate malazi.

"Mpaka sasa tumefikia hatua nzuri katika ujenzi wa bweni na endapo wadau wangeweza kutuchangia japo vifaa hivyo basi tungeweza kuanza na angalau wanafinzi 80." Ameongeza.

Akielezea siri ya mafanikio ya NAPS kufanya vizuri kitaaluma, mwalimu wa shule hiyo Raban Kijanjali amesema kuwa watoto si tu wanaandaliwa kitaaluma bali huandaliwa kiroho pia ili kuwajengea nguvu ya Mungu pindi wanapokuwa masomoni.

"Shule yetu ipo chini ya kanisa Anglikana hivyo wanafunzi wanalelewa kiroho na kimaadili jambo linalochangia kuwaongezea nguvu katika masomo yao sanjari na tabia njema shuleni na wawapo nyimbani. Kiukweli kila mzazi anayependa mtoto wake kupata elimu na malezi bora anatamani kumleta mwanae NAPS lakini tumekwama ujenzi wa mabweni",amesema Kijanjali.


Mchango huo kutoka kampuni ya Wazalendo, ni matokeo ya utekelezaji wa ahadi aliyotoa Bwana Ruhundwa wakati wa mahafali ya darasa la saba yaliyofanyikia shuleni hapo hivi karibuni.

Wazalendo ni kampuni inayojishughulisha na shughuli mbalimbali hasa kuandaa matamasha, kuzalisha na kusambaza simulizi na vipindi vya TV na Radio, kupokea na kutembeza watalii, mavazi na fashion n.k.

NAPS ni shule inayomilikiwa na kanisa Anglikana Dayosisi ya Kagera ambayo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma mkoani Kagera. 

Shule hii inasifika pia kwa kuwa na gharama ndogo sana ya ada.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com