Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,Simon Haule
**
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Masesa Sesaguli mkazi wa kitongoji cha Mwakakongoro kijiji cha Butini kata ya Itwangi katika wilaya ya Shinyanga anadaiwa kumuua kwa kumpiga kwa fimbo mtoto wake wa kike Nshoma Masesa (16) mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Sekondari Buhongwa iliyoko mkoani Mwanza.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Oktoba 1,2017 ambapo mwanafunzi huyo aliuawa kwa kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi katika kijiji cha Butini.
Mashuhuda wa tukio hilo waliieleza Malunde1 blog kuwa mwanafunzi huyo ameacha shule mwaka huu kisha kutoroshwa na mwanaume huko Kahama ili akaolewe ndipo mzazi wake (Masesa Sesaguli) alipoamua kumfuata kisha kumwadhibu kwa kumchapa fimbo mpaka akapoteza maisha
"Baba wa mtoto hakuweponyumbani aliporudi nyumbani akakuta taarifa mtoto wake ameacha shulena ametoroshwa na mwanaume “amepulwa” ,kaenda kuolewa Kahama,ndipo akaamua kumfuata",waliongeza mashuhuda.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Simon Haule alisema chanzo cha mauaji hayo ni mwanafunzi huyo kutoroshwa shuleni na kupelekwa kwenda kuishi Kahama.
Alisema baada ya binti huyo kutafutwa na kurejeshwa nyumbani kwao, ndipo baba yake huyo akaanza kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake, hadi kufikia hatua ya kuishiwa nguvu na kupoteza maisha, na baada ya tukio hilo mwanaume huyo alitoroka kusikojulikana.
Hata hivyo Kamanda aliwataka wazazi kutokuwa na hasira wanapoadhibu watoto huku akiwaasa wanafunzi wa kike kujikita zaidi kupenda masomo ili kutimiza malengo yao na kuacha tabia ya kujiingiza kwenye masuala ya mapenzi wakiwa na umri mdogo, ambayo yamekuwa yakiwaharibia mwelekeo wa maisha yao.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog