Picha : MIFUPA YA BINADAMU YAKUTWA KWENYE BWAWA LILILOKAUKA LA TINDE - SHINYANGA



Mifupa inayodaiwa kuwa ni ya binadamu imekutwa katika bwawa la Tinde lililopo katika kijiji cha Nyambui kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga ambalo sasa limekauka kutokana na ukame.

Mifupa iliyokutwa ni pamoja na fuvu la kichwa,mfupa mmoja wa mguu sehemu ya paja,mfupa mmoja wa mguu chini ya goti,mifupa miwili ya mkono,taya moja ya upande wa chini,mfupa mmoja wa sehemu ya bega na mifupa 14 ya mbavu.

Inaelezwa kuwa tukio hilo limetokea leo saa 11 jioni Jumatatu Oktoba 9,2017 wakati wananchi wakichimba kisima ndani ya bwawa hilo ambalo limekauka. 

“Kutokana na tatizo la ukame,wananchi walikuwa wanachimba kisima kwenye bwawa ambalo hivi sasa limekauka,wakati wanaendelea kuchimba ndiyo wakaona mifupa ya binadamu,hatujajua huyo mtu alifariki kwa njia gani,pengine alitumbukia kipindi bwawa lina maji ama alifukiwa na watu wasiojulikana”,kilieleza chanzo cha habari cha Malunde1 blog. 

Mkuu wa kituo cha polisi kituo cha Tinde pamoja na mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga,mheshimiwa Azza Hilal (CCM) wamefika eneo la tukio. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari,Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule amesema baada ya kupatikana kwa taarifa hizo jeshi la polisi lilichukua hatua za haraka na kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa awali kwa kushirikina na daktari mtaalamu wa viungo vya binadamu.

Amesema uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kufuatilia na kupata taarifa kamili kutoka ofisi ya mganga mkuu mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga,kufuatilia kumbukumbu mbalimbali za polisi ili kuona kama kuna taarifa ya mtu yeyote aliyepotea au kufa maji bila kujulikana au kuuawa katika mazingira tatanishi.

Amesema hatua nyingine waliyoichukua ni kufungasha sampuli zote muhimu za mifupa hiyo kwa ajili ya kuipeleka kwenye ofisi ya mkemia mkuu wa serikali anayeweza kubaini vinasabana jinsia ya binadamu husika.

Hata hivyo amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mifupa hiyo inadhaniwa kuwa ardhini kwa muda wa takribani miaka mitano iliyopita.

Mwakilishi wa Malunde1 blog – Tinde,Said Nassor ametutumia picha kutoka eneo la tukio,Tazama hapa chini
Mifupa inayodaiwa kuwa ni ya binadamu iliyokutwa kwenye bwawa la Tinde
Mifupa hiyo
Shimo ambamo kumekutwa mifupa
Wananchi wakishangaa
Wananchi wakishangaa mifupa hiyo
Mwananchi akishangaa mifupa hiyo
Mwananchi akikusanya mifupa hiyo
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Shinyanga Azza Hilal,mkuu wa kituo cha polisi Tinde na wananchi wakiwa eneo la tukio
Sehemu ya bwawa la Tinde likiwa limekauka

Bwawa likiwa limekauka

Picha zote na Said Nassor - Malunde1 blog - Tinde

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post