Imeelezwa kuwa maeneo ya Kata ya Ngokolo na Ibadakuli katika mtaa wa Bugweto manispaa ya Shinyanga yanaongoza kwa vitendo vya kihalifu hali ikiwemo vitendo vya wizi,uvunjaji,ubakaji na ukabaji hali inayotishia usalama wa raia na mali zao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa polisi wilaya ya Shinyanga,Claud Kanyorota (pichani) wakati wa mkutano wa jeshi la jadi sungusungu ‘Sanjo’ wilaya hiyo uliofanyika katika kata ya Mwamalili katika manispaa ya Shinyanga mwishoni wa wiki iliyopita.
Kanyorota alisema maeneo yanayoongoza kwa uhalifu katika wilaya ya Shinyanga ni Ngokolo na Bugweto ambapo aliuomba uongozi wa sungusungu kuhuisha jeshi la sungusungu kwenye maeneo hayo ili kutokomeza vitendo hivyo.
“Haya maeneo ya Ngokolo na Bugweto bado yanasumbua,na tumebaini kuwa maeneo yana shida sasa hivi ni yale ambayo pengine sungusungu imelega lega au haipo na tumekubaliana kuhuisha sungusungu ili kutokomeza vitendo hivyo”,alisema Kanyorota.
“Hawa wahalifu hawakai vichakani,hawa ni watoto wetu,wapangaji wetu,ni lazima tuje na mkakati wa kuhakikisha kuwa tunapiga ufagio katika mitaa,vijiji na kata zote na kusiwe na kata legelege ambayo itakuwa kimbilio la wahalifu”,alieleza Kanyorota.
Aliliomba jeshi hilo kwa kushirikiana na jeshi la polisi kuwashughulikia wahalifu kwani wanahatarisha amani katika jamii.
“Napenda kuwaita sungusungu kuwa nyinyi ni wapelelezi namba moja,kwa sababu popote alipo mtu,sungusungu yupo na popote penye uhalifu sungusungu yupo,kumbukeni kuwa mna dhamana ya kulinda amani katika jamii,naomba mtimize wajibu wenu”,alisema.
“Sheria inawatambua kuwa jeshi la sungusungu kuwa mpo kwa ajili ya kusaidia kuleta amani katika nchi yetu,katiba yetu inakata mtu kuua,mnapokamata mhalifu mfikisheni katika vyombo vya dola hivyo mnatakiwa kufanya kazi yenu kwa kuzingatia sheria za nchi”,alisema Kanyorota.
Aidha aliliwataka sungusungu kutumia njia za kistaarabu katika kumaliza uhalifu ambapo alilisisitiza jeshi hilo kutoza faini zinazoendana na hali ya uchumi wa wahalifu kwani faini kubwa zinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Katibu Mkuu wa Sungusungu wilaya ya Shinyanga ya Shinyanga James Deshi tayari wamehuisha jeshi la sungusungu kwenye maeneo ya Ngokolo na Bugweto na wapo tayari kushughulika na wahalifu.
Aidha alisema ushirikiano kati ya jeshi la sungusungu na polisi hivi sasa ni mzuri.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo alilipongeza jeshi la sungusungu kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi na kuwataka kushirikiana zaidi ili kulinda amani ya nchi.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog