Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MATIRO: SUNGUSUNGU TUMIENI FAINI ZA WAHALIFU KUFANYA MAMBO YA MAENDELEO


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine amelitaka jeshi la jadi sungusungu kutumia faini na michango wanayochangiana kufanya masuala ya maendeleo ikiwemo kununua vyombo vya usafiri ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri badala ya kusubiri kuchangiwa.

Mkutano "Sanjo" hiyo imefanyika Septemba 30,2017 katika shule ya Msingi Ujamaa iliyopo katika kijiji cha Seseko kata ya Mwamalili katika manispaa ya Shinyanga.

Matiro alisema jeshi la sungusungu limekuwa likitoza faini wahalifu katika jamii lakini fedha hizo hazitumiki kufanya mambo ya maendeleo yanayoonekana.

“Mimi ninachokujua ni kwamba jeshi la sungusungu lina pesa nyingi,na pesa hizo zinatokana na michango na faini,mnapata pesa lakini hazionekana kutumika kufanya vitu vinavyoonekana,tuweke mikakati ya kutumia fedha zile kufanya mambo ya maendeleo,ikiwemo kununua vyombo vya usafiri”,alisema Matiro.

Alilitaka jeshi hilo kutumia faini zinazopatikana linunue vyombo vya usafiri badala ya kutegemea serikali iwaletee usafiri.

“Wananchi wanalalamika kuwa mnatoza faini kubwa,pesa zinaonekana kutofanya vitu vya maendeleo yanayoonekana,Mimi nina uhakika mkiweka mikakati kwa kila tarafa,kwa zile faini zinazopatikana tuanze kuweka lengo la kununua pikipiki,hili suala nawaachia ili mjadili kwenye vikao vyenu”,alieleza.

Katika hatua nyingine alilitaka jeshi hilo kufuata sheria za nchi katika kutekeleza majukumu yao na kuacha kujichukulia sheria mkononi kama vile kuua watuhumiwa wa vitendo vya uhalifu na badala yake wawafikishe kwenye vituo vya polisi.

Aidha Matiro alilipongeza jeshi la jadi sungusungu kwa ushirikiano linaloutoa katika kukomesha vitendo vya kihalifu katika jamii na kwamba serikali inalitambua jeshi hilo na itaendelea kushirikiana nalo katika kuimarisha ulinzi na usalama katika jamii.

Mkuu huyo wa wilaya alitumia fursa ya mkutano huo kuliomba jeshi la sungusungu kuhimiza wananchi kupanda miti ili kukabiliana na hali ya jangwa mkoani Shinyanga sambamba na kulima zao la pamba.

Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu wa Sungusungu wilaya ya Shinyanga ya Shinyanga James Deshi alisema changamoto kubwa inayowakabili hivi sasa ni usafiri hivyo wanahitaji pikipiki ili ziwasaidie katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com