Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe alipotangaza kwamba ameunda wizara mpya ya kuangazia usalama mtandaoni na kutambua hatari pamoja na kuchukua hatua, raia walianza utani.
Kuna ilani bandia iliyoanza kuenezwa mtandaoni ambayo ilikuwa na sahihi bandia pamoja na nembo ya waziri huyo mpya Patrick Chinamasa.
Katika barua hiyo, waziri huyo alikuwa amewaagiza wanachama wote wa makundi ya WhatsApp kuhakikisha wamejisajili katika wizara hiyo kufikia Novemba.
Kwenye sahihi yake, palikuwa pameandikwa "Kwa Kutumia Mamlaka ya Mtandaoni Niliyopewa."
Lakini utani huo sasa umepungua, na raia wa Zimbabwe sasa wanajadili matokeo ambayo wizara hiyo itakwua nayo kwa uhuru wa raia - sana uhuru wa kujieleza.
'Tishio kwa dola'
Serikali ya Zimbabwe imekuwa na wasiwasi sana kuhusu mitandao ya kijamii tangu mhubiri Evan Mawararire salipoongoza kampeni ya #ThisFlag mwaka jana.
Alitumia mitandao kama vile Twitter na Facebook kuandaa maandamano ya watu kususia kazi, ambayo yalikuwa makubwa zaidi dhidi ya serikali katika kipindi cha mwongo mmoja.
Msemaji wa Rais Mugabe, George Charamba, amesema Mugabe alipata wazo la kuwa na wizara mpya ya kukabiliana na "tishio dhidi ya dola...tishio ambalo linatokana na vitendo vilivyo kinyume cha sheria."
Mitandao ya kijamii imekuwa nyenzo muhimu kwa raia nchini humo kuwasiliana na kupokea habari.
Wengi wanaitumia licha ya sheria kali zinazokandamiza uhuru wa kujieleza.
Kwa miaka 16 iliyopita, matumizi ya mtandao wa intaneti yameongezeka pakubwa nchini humo, kuanzia 0.3% hadi 46% kwa sasa, kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Teknolojia ya Mawasiliano (ITU).
Vituo kadha vya TV pamoja na majarida ya mtandaoni, baadhi ambayo hufanya kazi ya uanahabari kutoka nje ya nchi, nhusambaza habari kwa kutumia intaneti.
Maandamano ya #ThisFlag yaliathiri shughuli Harare
Vituo vya mafuta vilipoishiwa na mafuta ya petroli mwezi uliopita, kulikuwa na foleni ndefu katika maduka ya jumla raia wa Zimbabwe wakinunua vyakula kwa wingi na kujihifadhia wakidhani kungekuwa na uhaba mkubwa wa vyakula.
Serikali, baada ya kutiwa wasiwasi na matukio hayo, ililaumu ujumbe kwenye mitandao ya kijamii.
"Mitandao ya kijamii ilitumiwa vibaya kuzua wasiwasi, na hivyo kuyumbisha uchumi," anasema Bw Charamba.
Waziri mpya wa usalama wa mitandao Bw Chinamasa anakubaliana na msemaji huyo wa rais.
Kabla ya uteuzi wake, alisema "chanzo cha haya yote ni mitandao ya kijamii."
"Hii ina maana kwamba hili ni suala la kiusalama. Kuna ajenda ya kisiasa, na ajenda ya kutaka kubadilisha serikali. Tutachunguza kwa makini kujua nini hasa kilitokea kwa lengo la kuchukua hatua za kurekebisha hali kiusalama."
Upinzani na watetezi wa haki za kibinadamu hata hivyo wanatazama hatua hiyo kama juhudi za kuminya uhuru wa raia.
Chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) kinadai wizara hiyo mpya ni njama ya serikali kuwapeleleza zaidi raia wake.
Kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai anaamini wizara hiyo imeundwa kuwanyima raia uhuru wa kujieleza kabla ya uchaguzi wa 2018.
Raia wa Zimbabwe wameendelea kufanyia mzaha waziri huyo na kumuita "Waziri wa WhatsApp".
Wengine hata hivyo wana msimamo tofauti na wanaamini hilo linaonyesha ukosefu wa ufahamu kuhusu uhalifu wa kimitandao.
Wengine wanaamini kuna uhusiano kati ya hilo na uchaguzi mkuu ujao.
Social Plugin