Waziri wa Nishati, Medard Kalemani amemtaka Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Abdallah Ikwasa kumuondoa mara moja meneja uendeshaji wa kituo cha umeme Kidatu akituhumiwa kwa uzembe.
Dk Kalemani amesema hayo leo Alhamisi Oktoba 26,2017 baada ya kukosekana umeme nchi nzima jana Jumatano Oktoba 25,2017 kwa takriban saa 10, huku kukiwa hakuna ufafanuzi wa kueleweka.
Waziri amemtaka meneja huyo kuandika barua ya kujieleza ndani ya saa tatu ni kwa nini asiondolewe katika nafasi hiyo.
Dk Kalemani pia amempa siku tatu Meneja Udhibiti wa Mitambo, Mhandisi Izihaki Mosha kujieleza ni kwa nini anastahili kubaki katika nafasi hiyo.
Mbali na maagizo hayo, waziri amemtaka Ikwasa; Naibu Mkurugenzi Usafirishaji, Mhandisi Bishaija Kahitwa na Mosha kuandika barua za kuachia nafasi zao iwapo umeme hautarudi siku nzima leo.
“Siwaondoi, bali nataka umeme usiporudi muondoke wenyewe katika nafsi zenu kwa sababu hii kazi itakuwa imewashinda,” amesema.
Dk Kalemani amesema, “Haiwezekani umeme ukatike nchi nzima ndani ya saa 10 na bado hamjajua tatizo ni nini, wananchi wanatuma ujumbe mfupi kila kona wameunguliwa vitu vyao, wameunguliwa mashine zao nani atalipa hizo gharama.”
Waziri aliyefanya ziara kwenye mitambo ya kuzalisha umeme Ubungo na Kinyerezi I jijini Dar es Salaam kubaini chanzo cha kukatika kwa umeme nchi nzima, amesema wakati wa kufanya kazi kwa mazoea umekwisha.
Amesema haiwezekani kusiwe na spea za akiba za mitambo ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa umeme.
Dk Kalemani amehoji iwapo kulikuwa na hitilafu kwenye gridi ya Taifa ni kwa nini mashine nyingine nazo zipoteze mwelekeo huku kukiwa na kitengo cha mfumo wa uendeshaji.
“Hakuna haja ya kuwa na mfumo ambao hautoi taarifa mapema kama kuna tukio hatarishi linakuja, ninachotaka kusikia ni nini kifanyike ili tuwe na taarifa mapema,” amesema.
Waziri amesema, “Kila mnaloulizwa hamjui, mnasubiri hadi mitambo iharibike ndipo mchukue hatua, nchi haiwezi kuendeshwa hivyo, kukosa umeme ndani ya saa 10 ni hatari kwa mali za raia lakini kwa usalama pia. ”
“Sitaki kubishana hilo ndilo neno ninalowaacha nalo leo, nataka umeme urudi nchi nzima, hii haiwezekani,” amesema Dk Kalemani.
Pia, ameagiza mkandarasi anayeshughulikia mfumo wa utendaji wa umeme ambaye yupo nje ya nchi kurudi nchini.
“Nataka awepo kazini kesho na sitaondoka kuelekea Dodoma hadi nijue hatima ya mkandarasi, ” amesema.