Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire jana aliachiwa na Polisi waliokuwa wakimshikilia kwa masaa kadhaa tangu asubuhi.
Akizungumza baada ya kuachiwa na polisi baada ya kuhojiwa kwa saa saba jana, Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire, alisema hatua hiyo inatokana kutuhumiwa kutaka kuhatarisha msafara wa Rais Dk. John Magufuli wakati akiwasili Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
“Nikiwa uwanjani nilifuatwa na askari wawili ambao waliniambia nipo chini ya ulinzi.
“Niliwauliza tatizo ni nini wao walinijibu wamepewa maelekezo kutoka juu kisha walinipeleka kituo kidogo cha polisi uwanjani na kuniweka hapo.
“Baada ya rais kuondoka uwanjani nilichukuliwa na askari wengine watatu ambao walinipeleka kituo kikuu,” alisema.
Alisema askari hao waliomfuata uwanjani walimchukua kwa gari dogo binafsi na alipofikishwa kituo kikuu cha polisi katika ofisi ya RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa), walimueleza kuwa wamearifiwa kuwa alikuwa ameandaa kitu kibaya kwenye msafara wa rais kitendo ambacho alidai kilimsikitisha.
“Walipomaliza kunichukua maelezo niliendelea kukaa pale nje ya ofisi yao na ndipo alipokuja RCO na kuniita ofisini kwake ambako alinieleza kwamba shida iliyopo ni ‘sisi kwa sisi tunasigana’.
Aliniambia: “Nyie kwa nyie mnavutana mnatupa kazi ngumu sisi watendaji, kisha akaniruhusu nidhaminiwe na kutoka”.
Kauli ya Rais Magufuli
Akizungumzia jana suala la Meya huyo kukamatwa, Rais Magufuli alisema ameyaona mabango likiwamo lililokuwa limeandika kuwa Meya wa jiji la Mwanza, James Bwire, amewekwa ndani na Mkuu wa Mkoa ili asionane na rais.
Rais Magufuli aliwataka viongozi wa Mwanza kuacha malumbano na kukaa meza moja kumaliza mambo yao kwa kuwa wanatoka chama kimoja.
Alisisitiza kwamba wakiendelea na tabia hiyo hawatafika popote.
“Mkiendelea kulumbana mtashindwa kutatua kero za wananchi, haya mabango ya mara kwa mara yanatokea kwa sababu mnashindwa kutatua matatizo yao.
“Wajane wanadhulumiwa na masikini hivyo hivyo, tambueni mkishindwa kutatua mgogoro mapema, utawashinda ukikaa muda mrefu,” alisema.