Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire anashikiliwa na Polisi ikidaiwa ni kutokana na agizo la mkuu wa mkoa huo, John Mongella.
Hata hivyo, Mongella amekana kuamuru kukamatwa kwa kiongozi huyo anayeshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Jiji la Mwanza.
Mariam Lima ambaye ni katibu wa mitandao ya taasisi ya Alliance inayomilikiwa na meya Bwire amesema kuwekwa kwake ndani kunatokana na agizo la mkuu wa mkoa.
“Nimepata taarifa za meya kuwekwa mahabusu; mimi sihusiki na ninazifuatilia kujua kinachoendelea,” amesema Mongella leo Jumatatu Oktoba 30,2017.
Taarifa zinasema meya Bwire amekamatwa katika Uwanja wa Ndege Mwanza wakati wa mapokezi ya Rais John Magufuli ambaye ziko ziarani mkoani humo.
Lima amesema, “Tunafanya jitihada za kumwekea dhamana ingawa tunakabiliana na changamoto nyingi.”
Tangu Aprili, Bwire na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba wamekuwa katika mgogoro kila upande ukiutuhumu mwingine kuhujumu shughuli za maendeleo.